Tuesday, 1 May 2018

Manispaa ya Ilemela yajipanga kuwafikishia wananchi huduma ya Maji

Judith Ferdinand, 
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mkoani Mwanza MWAUASA, inatarajia kutekeleza kutekeleza miradi mbalimbali ya maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
Akizungumza jana katika kikao cha robo mwaka cha Baraza la Madiwani, Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Amosy Zephania alisema katika mwaka wa fedha 2017/2018 wametekeleza miradi mbalimbali ya maji na wanatarajia kutekeleza kwenye maeneo mengi wakishirikiana na MWAUWASA ikiwemo ujenzi wa tanki lenye lita za ujazo 500, mabomba yenye urefu wa mita 11,640 na uwekaji pampu ya kusukuma maji “booster” katika maeneo ya Ibanda Juu, Ibanda Ziwani, Ibanda Busisi, Mihama na Jiwe Kuu huku jumla ya wanufaika 336  wakiunganishwa bure.
Alisema katika ujenzi wa tanki lenye mita za ujazo 1,200 mabomba yenye urefu wa mita 20,530 na uwekaji wa pampu ya booster katika maeneo ya Nyasaka, Nsumba, Kiseke, Nundu, Buhilya, Kangae Kaskazini ambapo jumla ya wanufaika 632 wataunganishwa bure.
Alisema mradi wa ujenzi wa tanki lenye mita za ujazo 1,200 mabomba yenye urefu wa mita 9,450 na uwekaji wa pampu ya booster katika maeneo ya Kiloleli B, Nyamanoro Mashariki na Kilimahewa wanatarajia jumla ya wanufaika 1,065 wataunganishwa bure.
Aliongeza kwamba wanatarajia kubadilisha mabomba katika maeneo ya Kirumba yenye urefu wa mita 8,280 na kujenga chanzo kipya cha maji katika eneo la Sangabuye chenye uwezo wa kuzalisha lita za ujazo milioni 40 kwa siku ambapo maeneo ya Sangabuye, Igombe, Bugogwa, Kabusungu na Buswelu watanufaika na mradi huo ambao mpaka sasa uko katika hatua za mwisho za usanifu.
Hata hivyo alisema mradi ambao haujaanza kutekelezwa ni wa ujenzi wa bwawa la maji taka lenye uwezo wa kuhifadhi lita za ujazo 12,500 kwa siku katika maeneo ya Buswelu na Nyamhongolo pamoja na kuongeza mtandao wa maji taka mita 843 katika maeneo ya Kilimahewa, Bigbite, Msuka na Mji Mwema ambapo mradi umekamilika.
Alibainisha kwamba takribani nyumba 1,000 zimeunganishwa na mfumo wa kuondoa maji taka katika maeneo ya milimani yenye urefu wa mita 1,750 ambapo mradi huo umefanyika Kilimahewa A na B pamoja na kubadili mabomba ya maji taka, ujenzi wa chujio la uchafu, ufungaji wa pampu za maji tatu eneo la Kirumba.
Vilevile alisema mbali na hayo, pia wameweza kujenga vyoo katika shule za msingi Sima, Kitangiri C, Bondeni, Kilimahewa, Nundu A, Gedeli, Nundu D, Ziwani, Bulola, Kitangiri A, Pasiansi na Busweli pamoja na maeneo ya soko la Nyakato National na Buswelu, zahanati ya  Nyakato na Nyerere.
Kwa upande wake Diwani wa Viti Maalum Ilemela (CCM), Denisa Pagula alisema chanzo cha maji Sangabuye na mabwawa yanahitaji fidia hivyo alimuomba Meya wa halmashauri hiyo kusaidia ili  miradi hiyo iweze kutekelezwa na lengo ni kumsaidia mwanamke kutua ndoo kwa kupata maji kwa urahisi ikiwa ni kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Pagula alisema mradi wa maji taka usambae maeneo ya milima ili kusaidia kuondoa magonjwa ya mlipuko kwa wananchi wa maeneo hayo ambao vyoo vyao siyo vizuri na wanatiririsha maji taka mvua zinaponyesha.
Naye Diwani wa Kata ya Buswelu (CCM), Sarah  Ng’ hwani aliiomba MWAUWASA kusaidia kutatua changamoto kwa kujenga vyoo shuleni ili watoto wasome katika mazingira salama kwani hali ya halmashauri hiyo ilikuwa mbaya

No comments:

Post a Comment