Monday, 23 April 2018

Mahakama Yamwachia Huru Nabii Tito


Mahakama  ya Wilaya ya Dodoma, imemfutia mashtaka ya kutaka kujiua na kuamuru akapatiwe matibabu ya afya ya akili katika Taasisi ya Mirembe Isanga, mkazi wa mtaa wa Ng’ong’ona Manispaa ya Dodoma, Onesmo Machibya (44), maarufu kama ‘Nabii Tito’.

Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo baada ya kupokea ripoti za vipimo vya afya ya akili ya Nabii Tito kutoka Mirembe Isanga, vinavyothibitisha kuwa ana ugonjwa wa akili.

Awali, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, James Kalayemaha, aliagiza kuwa Nabii Tito apelekwe katika taasisi hiyo ya magonjwa ya akili ili kupatiwa matibabu ya afya ya akili na mahakama imemwondelea mashitaka yaliyokuwa yakimkabili.

Alisema katika ripoti ya kitabibu inaonyesha kuwa Nabii Tito kweli ana matatizo ya afya ya akili, hivyo anatakiwa kupelekwa katika taasisi hiyo ya Isanga Mirembe ili kupatiwa matibabu.

Mahakama hiyo, Februari 5, mwaka huu, iliamuru kuwasilishwa kwa vielelezo vinavyoonesha Nabii Tito ana matatizo ya akili na kufanyiwa vipimo katika Taasisi ya Afya ya Akili Mirembe Isanga kutokana na mshitakiwa kudai kuwa ana matatizo ya akili.

Akitoa maelezo ya kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, James Karayemaha, Wakili wa Serikali, Beatrice Nsana, aliiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuwasilishwa kwa taarifa kutoka Isanga.

Kutokana na maombi hayo, Hakimu Karayemaha alimuuliza mshtakiwa kama amekuja na vielelezo kama alivyoamriwa na mahakama hiyo.

Mshtakiwa huyo alimwambia Hakimu kuwa ametekeleza amri hiyo na kwamba tangu amri hiyo itolewe amekuwa mahabusu na hajapelekwa kwenye taasisi hiyo ya Isanga.

Hata hivyo, Hakimu Karayemaha alisema mshtakiwa huyo amewasilisha vielelezo vyake kutoka Hospitali ya Taifa ya Mhimbili na kwamba mahakama inahitaji taarifa kutoka Taasisi ya Mirembe Isanga kama ilivyoagiza.

“Mahakama ilitoa amri apelekwe Taasisi ya Mirembe Isanga kwa mujibu wa kifungu namba 219 (2) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai,” alisema Hakimu hiyo.

Kifungu hicho kinasema kama mshtakiwa atabainika kuwa kweli ana matatizo ya afya ya akili, mahakama itaamua kuwa alivyofanya tukio hilo hakuwa na akili timamu hivyo hana hatia.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Karayemaha alimwamuru Mkuu wa Magereza ya Isanga kutekeleza amri ya Mahakama iliyotolewa ya kumpeleka kufanyiwa vipimo mshitakiwa huyo.

“Namwamuru Mkuu wa Magereza Isanga atekeleze amri ya mahakama ili taarifa za mshtakiwa ziletwe kwa tarehe itakayopangwa ambayo ni Machi 5, mwaka huu, tutataja kesi na kupokea taarifa ya vielelezo vya vipimo vyake kutoka Isanga,” alisema Hakimu.

Nabii Tito alikuwa anashtakiwa kwa kosa la kutaka kujiua kwa kujikata na wembe na kujijeruhi kwenye maeneo ya tumbo Januari 25, mwaka huu katika mtaa huo wa Ng’ong’ona alipokwenda kukamatwa na polisi.

No comments:

Post a comment