Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amevishika pabaya vyama vikuu vya siasa nchini CCM na Chadema baada ya kuhoji matumizi ya zaidi ya Sh19 bilioni.

Ripoti hiyo ya ukaguzi wa hesabu iliyoishia Juni 30, 2017 iliyowasilishwa bungeni wiki hii, inaonyesha kati ya vyama 19 vilivyopata usajili wa kudumu, tisa havikuwasilisha taarifa za fedha wakati sheria inataka viwasilishe ifikapo Septemba 30 kila mwaka.

Katika ukaguzi huo, CAG anahoji matumizi ya zaidi ya Sh7 bilioni kwa Chadema na zaidi ya Sh12 bilioni kwa CCM. CAG anasema katika ukaguzi walibaini kuwa chama tawala kimeendelea kuwekeza katika kampuni nne na mikopo yenye thamani ya Sh12 bilioni.

“Hata hivyo, tumejifunza kwamba mikopo hiyo haina faida yoyote iliyoonekana imeingia kwenye chama,” anasema CAG.

Pia imebainika kuwa Sh80 milioni zilitambuliwa kama mapato ya uwekezaji katika taarifa za fedha za CCM kutoka Jitegemee Trading Company Limited lakini hazikuwa na kiambatanisho kinachothibitisha kama ni gawio au kitu kingine.

CAG anasema CCM bila kuanzisha sera, uwekezaji wa chama hicho upo katika hatari ya kutumiwa vibaya na kwamba malengo yaliyowekwa yanaweza yasifikiwe.

CAG pia amebaini kupitia ukaguzi wa taarifa za fedha za CCM kwa mwaka 2016/2017 kuwa hazina taarifa za kutosha kuhusu mikataba, masharti, kiasi na sababu za kutoa msaada wa Sh455.9 milioni kwa Radio Uhuru.

Taarifa hiyo inaonyesha kuwa menejimenti ya CCM ilikopa na kuhamisha Sh337.1 milioni kutoka akaunti ya malipo ya pensheni kwenda akaunti ya katibu mkuu wa chama na kupokewa kwa stakabadhi namba 156424. 

Hata hivyo, kiasi hicho hakijarejeshwa hadi wakati wa ukaguzi na kwamba, matokeo yake ni uwezekano wa madai ya wafanyakazi wastaafu kutolipwa kwa wakati.

CAG anasema Aprili 11, 2015 Chadema iliingia makubaliano na mwanachama wake ili awakopeshe Sh2 bilioni kwa ajili ya shughuli za chama.

Hata hivyo, anasema hawakukuta nyaraka zinazoonyesha kiasi hicho cha mkopo walichokubaliana iwapo kilitolewa na kupokewa na chama husika. 

CAG anasema katika ukaguzi, alikuta ankara ya kodi (tax invoice) yenye namba 201508226 iliyotolewa Agosti 26, 2016 ya Sh866.6 milioni ambayo ililipwa na mwanachama kwa niaba ya chama kwa ajili ya mabango ya matangazo yaliyoletwa na mzabuni M/S Milestone International Co. Ltd.

Anasema nje ya deni hilo, Sh715 milioni zililipwa kwa mwanachama kama marejesho ya fedha iliyokopwa kulipia ununuzi wa mabango bila ya kuambatishwa makubaliano ya kisheria.

Pia, anahoji matumizi ya Sh2.3 bilioni ambazo ni makusanyo ya Chadema kwa wanachama wake kwa mwaka 2014/15 na 2015/16, fedha ambazo zinadaiwa kutopelekwa benki na matumizi yake kutotolewa kwa ajili ya ukaguzi.

Ripoti ya CAG inaonyesha kuwa Chadema ilifanya ununuzi wa Sh2.1 bilioni bila ushindani; malipo ya Sh240.1 milioni yenye nyaraka pungufu; na Sh558.9 milioni ambazo ni masurufu ambayo hayakurejeshwa.

Wakati wa ukaguzi, CAG anasema alibaini vyama vinne vya Chadema (Kanda ya Magharibi), NLD, Demokrasia Makini na ADC havina daftari la mali za kudumu, hali inayosababisha ugumu wa kujua mali za chama, aina yake, gharama na sehemu zilipo, hivyo kuziachia mali za chama kwenye hatari ya kutumika vibaya.

“Kukosa daftari la mali za kudumu ni kinyume cha Sheria ya Usajili wa Vyama vya Siasa inayovitaka vyama vilivyosajiliwa kuwasilisha kwa msajili tamko la mali zote kila mwaka” anasema CAG.

“Ninashauri vyama vya siasa viwe na madaftari ya mali za kudumu ambayo yanahuishwa mara kwa mara kutokana na ununuzi au mauzo ya mali,” inasema taarifa ya CAG.

Kuhusu malipo yenye nyaraka pungufu ya Sh735.978 milioni, CAG amebaini vyama vitatu kati ya tisa vilivyokaguliwa, vina malipo yenye nyaraka pungufu kinyume cha miongozo ya kiuhasibu pamoja na kanuni Na. 86 (1) na kanuni na. 95 (4) ya Kanuni za fedha za Umma za mwaka 2001 ambazo zinaelekeza kila malipo yawe yameambatanishwa na nyaraka sahihi.

Kutokana na upungufu aliobaini, vyama vya CCM na Chadema vimepewa hati zenye shaka huku Chama cha Wakulima (AFP), ADC, Demokrasia Makini, Chama cha Kijamii, NLD, Sauti ya Umma na TLP vikipata hati mbaya.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: