Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangala, amezitaka halmashauri zote nchini kuacha kupora maeneo ya hifadhi za misitu kwa kisingizio cha kilimo.

Rai hiyo aliitoa jana wakati akifungua mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wakala wa huduma za misitu Tanzania, uliofanyika mkoani hapa jana.

Dk. Kigwangala alisema halmashauri zote nchini zinatakiwa kuacha mara moja kuvamia na kupora maeneo ya hifadhi ya misitu kwa kisingizio cha uhitaji wa maeneo ya kilimo.

“Kuna baadhi ya halmashauri za mikoa ya Pwani zimewapa wawakezaji eneo la kilimo ndani ya msitu wa hifadhi na matokeo yake mwekezaji amekuwa akivuna misitu yetu,” alisema Dk. Kigwangala.

Aliagiza wakala wa huduma za misitu nchini kuhakikisha wanalisimamia agizo hilo.

Hata hivyo, alisema matumizi ya mkaa na kuni ni changamoto kubwa kwa uharibifu wa misitu nchini kutokana na watu wengi kutegemea nishati hiyo kwa matumizi ya nyumbani.

Kutokana na matumizi ya mkaa na kuni, inakadiriwa kuwa hekta 400,000 hadi 1,000,000 zinateketea kila mwaka.

Dk. Kigwangala alisema mabaraza ya wafanyakazi yanasaidia kuleta tija kwa watumishi wake mahali pa kazi na kupitia kikao hicho, waangalie mambo muhimu ya kujadiliana ili kupata majibu ya changamoto za kiofisi.

Aidha, aliwataka wakala wa misitu nchini kuhakikisha wanasimamia kujua idadi ya miti inayopandwa katika maneo mbalimbali.

“Hivi katika kampeni hizi za upandaji miti zilizoanzishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, mnaijua idadi yake kweli, mnajua miti mingapi ilikufa na iliyobaki ni mingapi? Naomba mhakikishe mnakuwa na hizo takwimu,” alisisitza Dk. Kigwangala.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dosantos Silayo, alisema jumla ya misitu 11 itahifadhiwa katika mwaka huu wa fedha katika wilaya za Chunya, Singida, Chamwino na Handeni.

Alizitaja wilaya zingine kuwa ni Nyasa, Buhigwe, Tunduru na Mkinga, lengo likiwa ni kuhifadhi bioanuai na mapito ya wanyama pori na hifadhi za maji.

Hata hivyo, alisema watumishi wa wakala huduma za misitu wanakabiliwa na changamoto za kujeruhiwa na wengine kupoteza maisha kutokana na kushambuliwa na majangili wanapokuwa kwenye doria za kutekeleza majukumu yao.

Alisema, kuna vijiji 228 vilivyoingia katika maeneo ya hifadhi nchini, lakini wanaendelea kuzungumza na wahusika ili kutatua migogoro hiyo.

Prof. Silaya alizitaja changamoto zingine kuwa ni uvamizi wa misitu kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu pamoja na usafirishaji haramu wa mazao ya misitu unatishia uwepo wa rasilimali hiyo kwa vizazi vijavyo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: