Tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Mkonda kuanzisha kampeni ya kuwataka wakina mama waliokimbiwa na Baba wa watoto wao kujitokeza ofisini kwake kupata msaada wa kisheria wadau mbalimbali wamejitokeza kutoa maoni yao wapo waliosifu hatua hiyo wengine wakiponda.

Kada wa Chama cha Mapinduzi ambaye alikua Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema, Patrobas Katambi amejitokeza na kuunga mkono hatua hiyo akisema Makonda yupo sahihi na mbinu ya kuwatangaza hadharani anayotumia ni kama ile ya kuwatangaza wakwepa kodi (Parade Horribles).

Katambi ambaye kitaaluma ni Mwanasheria amesema, kifungu cha sheria namba 166-167 kinaeleza kuwa itakuwa kosa la jinai endapo wazazi/mzazi ambaye ana wajibu wa kukaa na mtoto akashindwa kumtunza na kumpatia mahitaji yake ya msingi.

" Kanuni ya kipimo cha vinasaba (The Human DNA Regulation act) ya mwaka 2009 kifungu cha 25 kinataja mamlaka ambazo zinaweza kuomba vipimo vya vinasaba vifanyike ni pamoja na Mahakama, Wakili, Afisa ustawi wa jamii, Polisi, taasisi za utafiti, matabibu, Mkuu wa Wilaya na Mkoa, kwa hiyo nyie mnaohoji uhalali wa Makonda kufanya hivyo ni vema mkaenda sambamba na hiki kifungu.

" Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kifungu cha 129 (1), (2) kinasema ni wajibu wa Baba mzazi wa mtoto katika ndoa kumtunza na waliopatikana nje ya ndoa kifungu cha 5 kinasema , watoto wote ni sawa," amesema Katambi.

Kada huyo wa CCM amesema ni vema wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kumuunga mkono mkuu wao wa mkoa na kuwataka wanasiasa wanaojaribu kupotosha waache kufanya hivyo kwani anachokifanya Makonda ni msaada mkubwa kwa akina mama wengi wanyonge ambao wamekuwa wakiteseka kulea watoto peke yao bila msaada wa akina Baba.

" Unajua akina mama wanateseka sana kulea watoto kutokana na waume zao kuwakimbia na wengine kuwatelekeza, kinachofanywa na RC Makonda ni mfano wa kuigwa kwa viongozi wengine bila kujalisha itikadi zao za kisiasa, kidini. Wengine wanapaswa kuiga haya yanayofanywa ili kuendana na sera ya Rais wetu John Magufuli ya kutetea wanyonge," amesema Katambi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: