Kocha wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, amewashauri wanachama na mashabiki wa Simba kuweka uzalendo mbele kwa kuiunga mkono Yanga katika hatua ya makundi waliyoifikia ili kukuza soka la Tanzania.

Yanga imefanikiwa kutinga katika hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufanikiwa kuiondoa Wolaitta Dicha ya Ethiopia kwa jumla ya mabao 2-1. 

Julio alisema linapokuja suala la kitaifa utani uwekwe pembeni na watu wote waungane na kuwa kitu kimoja kwa lengo la kuusogeza mbele mpira wetu.

“Nimefurahi Yanga kuingia hatua ya makundi kwani imesaidia Tanzania kuendelea kusomeka katika ramani ya mpira, ukiangalia leo hii Tanzania tunasomeka kupitia wachezaji Samatta (Mbwana) na Msuva (Simon).

“Kwa hiyo kama wamepata nafasi hiyo ni fahari kwa Tanzania japokuwa kuna utani wao wa Simba na Yanga kwenye mitandao unaendelea ambao unaweza kuwa na faida au hasara kwa pande zote mbili. Kwa sasa tuangalie utaifa kwani itatusaidia.

“Utani wetu ubaki utani na linapokuja suala la kitaifa watu wote tuungane tuwe kitu kimoja na kuiunga mkono Yanga japokuwa kuna watu wengi wa Simba hawakupendezewa na hatua hiyo kufuatia utani wao wa Simba na Yanga,” alisema Julio.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: