KAMBI Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema imejipanga kumbana kwa hoja 15 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, atakapowasilisha bungeni mjini Dodoma leo hotuba ya makadirio ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha.

Mambo hayo ni pamoja na kutotungwa kwa kanuni za sheria mpya ya habari iliyotungwa mwaka 2016, kupotea kitatanishi kwa waandishi wa habari, kusajili magazeti kila mwaka, waandishi wa habari kulipia vitambulisho vya kitaifa kila mwaka na ufujaji wa mapato ya mechi za soka zinazochezwa nchini.

Zingine ni serikali kutotenga bajeti kusaidia maendeleo ya michezo, madai ya wasanii kutengenezewa matabaka na wenye ving'amuzi kutoza huduma hadi kwa vituo vya televisheni (TV) visivyopaswa kulipiwa.

Pia wasanii kuimba nyimbo zisizo na maadili na kuvaa mavazi yasiyoendana na utamaduni wa Kitanzania, kuvamiwa kwa viwanja vya michezo nchini na changamoto katika upatikanaji wa washindi wa shindano la Miss Tanzania.

Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Bunge la Bajeti iliyotolewa na Idara ya Habari na Elimu ya Bunge leo, Bunge litajadili kwa siku moja hotuba ya makadirio ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.

Akizungumza na Nipashe mjini hapa jana, Naibu Waziri Kivuli wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Devotha Minja, alisema wamepanga kuutumia mjadala huo kuibana serikali ili izitatue changamoto hizo.

Alisema hoja ya kwanza ni kile alichokiita kuvifunga midomo kwa vyombo vya habari vinavyomilikiwa na watu binafsi kwa kuvifungia na kuvitoza faini pale zinapochapisha au kutangaza habari kukosoa mwenendo wa utendaji wa serikali.

Alisema hali hiyo inarudisha nyuma maendeleo ya tasnia ya habari na kuminya uhuru wa kujieleza na haki ya kupata habari.

Minja ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), alisema hoja yao ya pili ambayo Dk. Mwakyembe watamtaka awape majibu bungeni leo ni kutotungwa kwa Kanuni za Sheria mpya ya Habari nchini.

Alisema licha ya Bunge kuipitisha muswada wa sheria hiyo na kutiwa saini na Rais takriban miaka miwili sasa, kanuni hazijatungwa ili ianze kutumika.

"Kwa sheria ile ambayo tuliipitisha, bado hazitengenezwa zile kanuni za kuunda mabaraza ya kushughulikia kesi za mwandishi mmoja mmoja," alisema Minja.

"Na hapa tunaona kuna ucheleweshaji wa makusudi ili sheria ya zamani iendelee kutumika kwa sababu inampa mamlaka waziri kufungia magazeti. Sheria ya sasa haina kitu kama hicho, inataka mwandishi aliyekosea ndiyo awajibike na si kufungia gazeti zima."

Minja ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari, pia alisema upinzani umejipanga kuutumia mjadala wa leo kumbana Dk. Mwakyembe ili wizara yake iachane na utaratibu wa waandishi wa habari kulipia kila mwaka Sh. 30,000 kupata vitambulisho vya kitaifa (press cards) badala yake wawe wanalipa kila baada ya miaka kuanzia mitatu hadi 10 kama ilivyo kwa leseni ya udereva na hati ya kusafiria.

Minja alisema malipo ya aina hiyo yako pia katika usajili wa magazeti, akieleza kuwa kuna utaratibu mpya umeanzishwa na wizara hiyo wa kusajili gazeti kila mwaka ambao hawauungi mkono.

Alisema utaratibu huo aliodai upo katika nchi mbili tu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaona si rafiki kwa uhai wa tasnia ya habari kwa kuwa umelenga kuyazima usajili magazeti yanayoandika habari zisizoifurahisha serikali.

Pia alisema watautumia mjadala wa leo kumbana Dk. Mwakyembe na serikali kwa ujumla kuhusu kile alichodai wasanii nchini wamegawanyika.

"Kuna wasanii wanapata upendeleo mkubwa wa serikali, na hili sasa limetengeneza matabaka kwa wasanii wetu. Yaani sasa tumefikia hatua wasanii wanakuwa wa chama fulani ilhali wanapaswa kuwa pamoja na kufanya kazi kwa kushirikiana," Devotha alisema.

Naibu waziri kivuli huyo pia alisema bado kuna changamoto ya ufujaji wa mapato ya milangoni kwenye mechi za soka nchini, akidai kuna Sh. milioni mbili zinadaiwa zinalipwa kwa wanaojiita wawezeshaji wa uwanja kwa kila mechi inayochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Sambamba na hayo, alisema watahoji bungeni sababu za uongozi wa Shirikisho la Soka (TFF) kuteua mtu mwenye tuhuma za rushwa kushika nafasi ya mtu aliyeondolewa madarakani kwa tuhuma zenye mwelekeo huo.

Aliongeza kuwa upinzani umejipanga kuibana serikali leo ichukue hatua stahiki dhidi ya watoa huduma za ving'amuzi ambao wamekuwa wakikata huduma hadi kwenye Tv zisizoruhusiwa kulipiwa nchini.

Wakati Minja akieleza hayo, Mbunge wa Wawi, Ahmed Juma Ngwali (CUF), alisema upinzani pia umejipanga kumbana Waziri Mwakyembe ili wizara yake iwe inatenga bajeti ya kusaidia maendeleo ya sekta ya michezo nchini.

Ngwali alidai kuwa kwa takribani miaka mitatu sasa, TFF haijawahi kupokea kiasi chochote cha fedha kutoka serikalini kusaidia maendeleo ya mpira wa miguu nchini.

Naye Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF), aliiambia Nipashe mjini hapa jana kuwa kama atapata nafasi ya kuchangia mjadala huo leo, ataitaka serikali kudhibiti maudhui ya nyimbo za wasanii na uvaaji wao.

"Nyimbo za wasanii wetu zinapaswa kuzingatia maadili. Mavazi yao pia ni lazima yazingatie utamaduni wetu ili kutunza heshima ya nchi," Sakaya alisema huku akisisitiza Baraza la Sanaa (Basata) linapaswa kuwajibishwa kwa kile alichodai limeshindwa kudhibiti wizi wa kazi za wasanii.

Mbunge huyo pia alisema atautumia mjadala wa leo kumshauri Dk. Mwakyembe na wizara yake kudhibiti udanganyifu katika upatikanaji wa washindi wa Miss Tanzania, akidai kuwa katika miaka ya karibuni shindano hilo limetawaliwa na udanganyifu.

"Miaka ya nyuma, nilifuatilia miaka mitatu ya mwanzo, mshindi ulikuwa unamwona kuanzia hatua ya mwisho kuwa huyu atashinda na kweli inakuwa hivyo. Lakini miaka ya karibuni kumekuwa na udanganyifu mkubwa ambao unaashiria ama rushwa au kujuana," alisema.

"Baadhi ya ma-Miss wenyewe wanaishi maisha ya ajabu ya kubadilisha wanaume. Hivi kweli hii ndiyo maana ya shindano hili? Kulikoni kuendelea kuiabisha nchi, ni heri lifutwe tu."

Sakaya pia alisema atautumia mjadala wa leo kuibana serikali ivirejeshe viwanja vya michezo na maeneo ya wazi yaliyovamiwa na kuendelezwa kwa kuwa uvamizi huo unakwamisha maendeleo yua watoto kimichezo.

"Ni aibu viwanja vya michezo vimevamiwa kujengwa majumba na serikali ipo inaangalia tu," alisema Sakaya na kuongeza:

"Ni lazima kama serikali inayojali maendeleo ya watoto na michezo tuvirejeshe viwanja na maeneo ya wazi yaliyovamiwa. Kama kuna mtu kajenga nyumba kwenye eneo la wazi tubomoe ili watoto wapate mahali pa kucheza.

"Lazima kama taifa tuwekeze katika michezo kwa sababu michezo ni ajira, ni afya na burudani. Rais mstaafu (Jakaya) Kikwete alikuwa analipa hadi mishahara ya makocha lakini sasa serikali inaonekana imejiweka kando kuendeleza michezo. Shuleni hakuna vifaa vya michezo.

"Tunategemea nini huko mbele kama hatuwekezi kwa watoto kwa sasa? Kina (Cristiano) Ronaldo hawakutengenezwa ukubwani, tuwekeze kwa watoto."
Share To:

msumbanews

Post A Comment: