Chemical.

THE Goethe Institut (Institute) ni taasisi iliyo chini ya Serikali ya Ujerumani. Ilianzishwa mwaka 1951. Makao makuu yake yapo jijini Munich, Ujerumani. Lakini ina matawi zaidi ya 150 katika nchi mbalimbali duniani.Dhumuni la kuanzishwa kwa taasisi hii ni kueneza na kufundisha utamaduni wa Kijerumani duniani. Pia kubadilishana tamaduni na mataifa mengine kupitia filamu, muziki na kazi mbalimbali za fasihi.

Hapa Bongo pia taasisi hii ina tawi na wanamiliki jengo lao pale Upanga jijini Dar. Jengo lao linaitwa Goethe Institut.
Sasa, Mei 19, 2016, katika jengo hilo, nilikuwa miongoni mwa waliofika kushuhudia uzinduzi wa Filamu ya Kitanzania iitwayo Bongo na Flava.
Filamu hiyo imeigizwa na wanamuziki wenye majina makubwa Bongo ambao ni One The Incredible, Fid Q, Wakazi, Lamar, Songa, Makamua, Salu T na Saigon. 

Ameshirikishwa pia Cheusi (wa Tamthiliya ya Siri ya Mtungi) na wengineo huku ikiwa imetayarishwa na kuongozwa na dairekta RlahC pamoja na prodyuza Karabani.
Nilipoitazama filamu hiyo, niligundua kuna wanamuziki Bongo wana vipaji na uwezo mkubwa wa kuigiza. Lakini pia picha ya wapi tasnia ya filamu nchini imetoka ilipanda kichwani kwangu.

Kimsingi ilianzishwa na wanamuziki Khaleed Mohamed ‘TID’, Juma Mchopanga ‘JayMo’ na baadhi ya waigizaji akiwemo Monalisa ambao walipata nafasi ya kushiriki katika Filamu ya Girfriend. Kwa hiyo, muziki na filamu ni vitu ambavyo vinaendana na wanamuziki wenye vipaji vya kuigiza wana nafasi ya kufanya makubwa hata kupiga pesa katika filamu endapo watajipanga.
Wema Sepetu

Tumeona katika mataifa yaliyoendelea ikiwemo Marekani, kuna wanamuziki wamefanya makubwa kwenye ulimwengu wa filamu. Wengi tunamfahamu Rapa DMX, ameigiza kwenye muvi nyingi zikiwemo Belly, Cradle 2 The Grave, Never Die Alone, Death Toll, Back Stage, Last Hour, Beef na nyingine nyingi.

Lakini hebu tazama kwa sasa namna ambavyo Rapa 50 Cent anavyopiga pesa kupitia filamu na tamthiliya kiasi kwamba yupo kwenye orodha ya Waigizaji 50 Bora Marekani kwa sasa. Muongoni mwa tamthiliya zilizompa mafanikio makubwa ni Power na filamu yake mpya ya Den Of Thief.

Hiyo ni baadhi tu ya mifano ambayo wanamuziki hapa Bongo wanaweza kujifunza. Kwamba, mbali na kukomaa na muziki tu, wanaweza kupiga pesa kupitia filamu.Jambo ambalo niliwahi kumweleza mwanamuziki Vanessa Mdee ‘Vee Money’ nilipopata nafasi ya kumuuliza juu ya mustakabali wake kwenye ulimwengu wa filamu na tamthiliya baada ya kupata nafasi ya kuigiza kwenye Tamthiliya ya MTV Sugar iliyoandaliwa na Kituo cha Televisheni cha MTV.

Vee alisema kuwa, hafikirii kuandaa muvi yake Kibongobongo kutokana na changamoto iliyopo ya soko la filamu. Sasa kama kila mmoja akiogopa changamoto ni nani atalinusuru soko hili?Inawezekana soko limedorora kutokana na waigizaji kushindwa kuwapelekea mashabiki wao vitu vipya vya kuwakosha, lakini wanamuziki, kwa kuingia kwenye filamu, wanaweza wakawa na kitu tofauti ambacho kitafufua amshaamsha ya watu kupenda filamu.

Binafsi nimpongeze msanii Chemical na menejimenti yake kwa kuthubutu kuandaa filamu iitwayo Mary Mary ambayo imempa nafasi mwanamuziki huyo kuonesha kipaji chake akiwa amemshirikisha mwigizaji mwenye jina kubwa Bongo, Wema Isaac Sepetu. Na kudairektiwa na Neema Ndepanya.‘Teaser’ ya filamu hii inaonesha kwamba ni filamu nzuri ambayo italeta mapinduzi kwenye suala zima la changamoto katika ulimwengu wa filamu nchini.

Ni jambo zuri. Kuona changamoto kama hizi zinaibuka kwenye filamu, lakini pia wanamuziki wakijichanganya huku na huko kuonesha nini wamebarikiwa na Mungu.Wanamuziki wanatakiwa kukumbuka kwamba wana faida ya mashabiki. Tayari wana mashabiki kwenye muziki ambao ninaamini wapo tayari kuwafuata hata kwenye filamu, kutazama wamefanya nini ikiwa wataamua kutumia fursa hiyo.

Mbali na hayo yote, tusubiri matokeo ya Filamu ya Mary Mary na namna itakavyopokelewa sokoni. Pengine itatoa majibu ya maswali magumu ambayo wanamuziki wamekuwa wakiwaza. Kwamba, wakiandaa muvi itakuwaje? Watapokelewaje? Watapata pesa? Mashabiki wao watawaonaje? Na maswali mengine kama hayo!

Stori: Boniphace Ngumije
Share To:

msumbanews

Post A Comment: