Diwani wa Viti Maalumu (CCM) afariki dunia


Diwani wa Viti Maalumu (CCM) wilaya ya Morogoro, Zuhura Mfaume amefariki dunia jana baada ya kuugua maradhi ya tumbo kwa muda mfupi na anazikwa leo, Tarafa ya Matombo wilayani humo.

Akitoa taarifa za kifo cha diwani huyo mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Sudi Mpili amesema Zuhura alifariki jana (Aprili 12) mtaa wa Karume Manispaa ya Morogoro ambako alikuwa akiugua kwa ndugu zake.

Mpili amesema kuwa marehemu Zuhura enzi za uhai wake alikuwa akiwasaidia sana akinamama na wananchi wa wilaya ya Morogoro kwa kuwawakilisha vyema katika vikao mbalimbali vya maamuzi.

Naye Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Kibena Kingo amesema kuwa marehemu Zuhura amedumu kwenye baraza la madiwani katika awamu mbili na alikuwa mtulivu na msikivu katika vikao mbalimbali.

Kingo amesema kuwa marehemu Zuhura alikuwa mtu mwenye msimamo na asiyeyumbishwa hivyo kila alichokuwa akichangia kilikuwa na mchango na mslahi kwa wananchi.

Kwa upande wake Diwani wa Viti Maalumu CCM, Jesca Mbondo amesema kuwa pengo aliloacha marehemu Zuhura haliwezi kuzibika kwani mbali ya kuwa diwani lakini pia alichukua nafasi kama mama na mlezi kwenye jamii na vikundi mbalimbali.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 komentar: