MKUU wa Wilaya ya Same, Rosemary Staki, amelazimika kuubeba mzigo wa kulipa gharama za kujiunga na bima ya afya kwa watoto 16 wenye ulemavu wa ngozi, baada ya kuelezwa hawana uwezo na wananyanyasika kupata huduma za afya.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuwatembelea watoto hao ambao wamechukuliwa na Shirika la Land Mark World Mission kwa ajili ya kusaidiwa kupata huduma muhimu za kibindamu.

“Najua kuna sera ya afya ya mwaka 2007 ambayo inaweza kulibeba kundi hili la watu wenye ulemavu kupata msamaha, lakini kwa sababu mpaka sasa hawajapata huo msamaha, mimi nawalipia watoto 16 ili waweze kufikia huduma za tiba katika hospitali zetu,” alisema.

Baada ya kuguswa na hali hiyo, baadhi ya wafanyabiashara na wadau wengine wa maendeleo walilazimika kumuunga mkono Mkuu huyo wa wilaya na kuwalipia Bima ya Afya iliyoboreshwa (iCHF), watoto wengine 23 wenye ulemavu na hivyo kufikia idadi ya wanufaika 39.

Kwa mujibu wa Staki, katika kuweka uwiano sawa kwa Watanzania wote bila ubaguzi, serikali ya awamu ya tano ina pendekezo la kutoa bima ya afya ya lazima kwa watu wote ambao utasaidia pia kwa watu wenye msamaha kupata huduma bora.

Hivi karibuni, serikali ilisema inafikiria kutoa huduma hiyo kwa kundi la watu wasio na uwezo na wenye mahitaji maalumu wakiwamo wazee na wenye ulemavu.

Hata hivyo, sera ya taifa ya afya imeainisha makundi maalumu yanayostahili kupata msamaha wa huduma za afya katika vituo vyote vya kutolea huduma kuwa ni wazee wenye umri zaidi ya miaka 60, watoto chini ya miaka mitano, waishio katika mazingira hatarishi, wajawazito na wasiojiweza kiuchumi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: