Sekta ya elimu katika mkoa wa Kigoma inakabiliwa na changamoto kubwa ya upungufu wa miundombinu ya nyumba za walimu, vyumba vya madarasa na upungufu wa walimu, jambo ambalo limekuwa chanzo cha kuporomoka kwa kiwango cha ufaulu wa wanafunzi na kudidimia kwa kiwango cha elimu mkoani humo.

Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Shirika la SODERA wakishirikiana na Twaweza mwaka 2015 inaonyesha kuwa katika wilaya ya Kasulu, asilimia 51 ya wanafunzi wa darasi la saba wanaweza kusoma kingereza cha darasi la pili kwa ufasaha huku asilimia 38 ya wanafunzi hao wanaweza kufanya hesabu za darasa la pili bila matatizo.   

Akizungumzia changamoto hiyo, Afisa elimu wa Shule za msingi wilaya ya Kasulu, Machozi Stephano alisema tatizo la wanafunzi kufeli halitokani na sababu za walimu bali zimekuwepo kutokana na mazingira mabovu ya kufundisha na kufundishia pamoja na miundombinu mibovu ya vyumba vya madarasa.

“Wanafunzi hasa wa vijijini wanatembea umbali mrefu kwenda shule na bado wakifika huko wanajikuta wakilundikana madarasani na wengine wanakaa muda mrefu bila kupata uji au chakula cha mchana, mwanafunzi wa aina hii kamwe hawezi kufaulu masomo na mitihani yake ya kitaifa,” alisema Stephano.

Alisema kuwa wilaya ya Kasulu ina upungufu wa walimu 2,010 ambapo kati yao shule za msingi zinahitaji walimu 735  na hivyo kufanya Mwalimu mmoja kufundisha wastani wa wanafunzi 113 katika chumba kimoja cha darasa.

“Baadhi ya wazazi wamebweteka na kauli ya elimu bule kwani wanaamini serikali itafanya kila kitu na wao kazi yao ni kununua sare za wanafunzi na madaftari. Ipo haja ya viongozi katika nafasi mbalimbali wakatoa ufafanuzi wa kina juu ya dhana hii ya elimu bule ili kila mmoja kwenye jamii akashiriki kikamilifu kuboresha sekta ya elimu ili mkoa wa Kigoma uweze kutatua changamoto zinazokabili sekta ya elimu,” alisema Stephano.

Baadhi ya wadau wa elimu katika wilaya hiyo waliilalamikia serikali kwa kushindwa kutatua changamoto hasa upande wa elimu ya msingi, jambo ambalo linasababisha elimu kuzidi kuporomoka kwa kasi na hivyo kushindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Mkazi wa mjini Kasulu, Ezra Edward alisema hakuna umuhimu wowote wa kutoa elimu bule kwa vile ubora wa elimu umekuwa ukishuka kwa kasi, badala yake fedha inayotumika kugharamia ada na mahitaji mengine ya shule na wanafunzi ni bora ikatumika kwa kuongeza walimu na kuboresha miundombinu ya elimu ili kuongeza ubora wa taaluma.

Alisema jitihada ya kukuza ubora wa elimu ya msingi bado inakabiliwa na changamoto ya utoro kwani aslimia 75 ya walimu ndio wanaohudhuria shuleni huku wanafunzi ni asilimia 71 tu, hivyo jamii haina budi kushirikiana pamoja ili kutokomeza utoro, jambo litakalosaidia kupata wasomi wazuri watakaosaidia kuleta maendeleo siku za zijazo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: