Friday, 13 April 2018

Baba amnywesha sumu mwanae


Mtoto wa miezi miwili (jina limehifadhiwa) mkazi wa Manispaa ya Shinyanga amedaiwa kunyeshwa sumu na baba yake mzazi kwa madai ya kutaka kuficha kizazi hicho ili mkewe asijue amezaa nje ya ndoa.

Akielezea makasa huo jana, mama mzazi wa mtoto huyo, Maria Shija (22) alisema lilitokea Machi 24, mwaka huu majira ya saa tatu usiku.

Maria alisema siku hiyo baba wa mtoto huyo, Edson Damian (37) alikwenda nyumbani kwao anapoishi yeye na mama yake kwa ajili ya kumsalimia mtoto huyo, na ndipo akamywesha sumu ya panya kwa lengo la kumuua wakiwa wamekaa nje.

Mzazi huyo alisema kabla ya mzazi mwenzake kufanya kitendo hicho, alikuwa akimtuma maji ya kunywa ndani mara kwa mara kitu ambacho si kawaida yake.

Alisema aliporudisha kikombe ndani mara ya mwishho ndipo akasikia harufu ya sumu ya panya, na aliporudi haraka kwa mtoto akamkuta ameanza kutoa mapovu na mwanaume huyo kukimbia.

“Baada ya kuona mtoto kapewa sumu nikakimbia kwa jirani ambaye ana zizi la ng’ombe, ndipo nikachukua maziwa nikamnywesha na baadae nikachukua bodaboda hadi kituo cha Polisi kupewa RB na kisha kwenda hospitali ya Rufani ya mkoa wa Shinyanga kupatiwa matibabu," alisema Maria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishina Msaidizi Simon Haule alithibisha kutokea kwa kisa hicho na kwamba mtuhumiwa huyo yupo mbaroni.

Alisema upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu shtaka linalomkabili.

Akielezea historia ya mapenzi yao, Maria alisema Damian wakati anamtaka kimapenzi alimwambia hana mke, lakini baada ya mtoto kuzaliwa akasema ana mke, hamtaki kwani atavunja ndoa yake.

Mtu wa karibu na familia ya Maria, Jumanne Kagusa alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: