Mabingwa wa soka nchini klabu ya Yanga, leo inaondoka jijini Dar es salaam kuelekea mkoani Morogoro, kwaajili ya kambi kujiandaa na mchezo wake wa robo fainali ya kombe la shirikisho dhidi ya Singida United.

Kikosi cha Yanga kinaondoka na wachezaji wake wote isipokuwa wale waliopo kwenye kambi ya timu ya taifa ya Taifa Stars ambayo inajindaa na mchezo wake wa kirafiki wa kalenda ya FIFA dhidi ya DR Congo kesho na watajiunga na timu baada ya mechi hiyo.

Wachezaji wanne wa Yanga waliopo katika kambi ya timu ya taifa ni kipa Ramadhan Kabwili, mabeki Hassan Kessy, Gadiel Michael, Kelvin Yondan pamoja na kiungo mshambuliaji Ibrahim Ajib.

Wapinzani wa Yanga, Simba wamekuwa wakiweka kambi yao Morogoro mara kwa mara. Yanga itakuwa Morogoro hadi Jumamosi ya Machi 31 ambapo itaelekea Singida kucheza na Singida United Jumatatu April 1 kwenye uwanja wa Namfua.

Baada ya mchezo huo Yanga inatarajiwa kurudi Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania tiketi ya hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika, dhidi ya Welayta Dicha ya Ethiopia Aprili 7 Uwanja wa Taifa.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: