Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa rai kwa wawekezaji wazawa na wafanyabiashara nchini kujenga viwanda vya dawa na vifaa vya tiba hapa nchini ili kuongeza kasi ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na kukuza ajira.

Rais Magufuli ametoa rai hiyo jana Jijini Dar es Salaam, kwenye hafla ya uzinduzi wa magari 181 yenye thamani ya shilingi bilioni 20.7 ya kusambaza dawa na vifaa vya tiba yaliyotolewa msaada na Shirika la Global Fund kwa Serikali ya Tanzania kupitia Bohari ya Dawa (MSD).

“Asilimia 94 ya dawa zinanunuliwa nje ya nchi, hivyo wawekezaji wazawa watumie changamoto hii kama fursa ya kuanzisha viwanda vya dawa na vifaa tiba hapa hapa nchini kwetu,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alibainisha kuwa ujenzi wa viwanda hapa nchini utasaidia kuongeza ajira kwa Watanzania hasa vijana pamoja na kupunguza gharama za kuagiza bidhaa nje ya nchi zikiwemo dawa na vifaa vya tiba.

Aidha Rais Magufuli alitoa wito kwa wataalamu na wasomi wazawa wa masuala ya afya na tiba kujiunga pamoja na kuanzisha viwanda vya dawa ili kuchochea uchumi wa viwanda na kuongeza mapato.

“Tunapoteza shilingi bilioni 500 kila mwaka kwa ajili ya kununua dawa nje ya nchi lakini tungekuwa na viwanda vyetu fedha hizo tungetumia kwenye mambo mengine ya maendeleo,” alisisitiza Rais Magufuli.

Pia Rais Magufuli alisisitiza kuwa madereva watakaoajiriwa kuendesha magari hayo mapya wachaguliwe kwa umakini ili kupata watu waaminifu watakaoweza kuyatunza kwa manufaa ya Watanzania.

Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) ilianzishwa mwaka 1994 kwa ajili ya kununua, kuhifadhi na kusambaza dawa na vifaa vya tiba nchini kote.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: