Na Mwamvua Mwinyi,Mkuranga
WATU 17 kati ya 26 waliofariki dunia katika ajali ya barabarani iliyotokea Mkuranga Mkoani Pwani ,wametambuliwa majina yao ambapo hatua inayoendelea ni kuwakabidhi kwa ndugu zao kwa ajili ya mazishi.
 
Aidha watu wengine kumi wamejeruhiwa na wamekimbizwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu.
 
Ajali hiyo imehusisha  gari  ndogo ya abiria aina ya Toyota Hiace yenye namba za usajili T.676 DGK inayofanya safari zake Kimanzichana – Mbagala Rangi na gari nyingine aina ya Lori.
 
Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Mkuranga, Stephen Mwandambo alisema amepokea maiti 25 na majeruhi hao ambapo majeruhi mmoja alifariki njiani wakati wakipelekwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
 
Mganga mkuu huyo aliwataja waliofariki na kutambuliwa majina yao ni 17 kati ya 26 waliofariki kuwa ni pamoja na  Selemani Guli (36) mkazi wa Kongowe,Modesta Sheleli (24 ) mkazi wa Vianzi,Doreen Selemani Seleli (5), sheila Hamad Mkuba ( 8 )mkazi wa Vianzi na Mariam Hussein Sadik (15 )mkazi wa Mwarusembe.
 
“Nassoro Hamis( 48) mkazi wa Jaribu Mpaka, Asha Athumani (24)mkazi wa Songosongo ,Nasma Athuman 22 Songosongo Mwanahawa Athuman (52),Mohammed Saidi (25) mkazi wa Njopeka na Mwajabu Jongo (20)mkazi wa Njopeka”;
 
Dokta Mwandambo aliwataja wengine ni Mwarami Mbunju(37) mkazi wa Mkamba na Abisaalom Uloga (25)mkazi wa Kimanzichana ,Kijongo Kibwana Jongo(26 )anakaa Jaribu Mpakani na Recho Japhet (16),Mariam Selemani (36)mkazi wa Mbagala  na Melania Kapatwa (38)mkazi wa Jaribu Mpakani. 
 
Inasemekana majeruhi waliopelekwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili wengine wamekatika viongo mbalimbali vya mwili.
 
Aidha dokta Mwandambo alisema wanakabiliwa na changamoto ya kipimo cha X-ray hali inayosababisha kushindwa kuwafanyia uchunguzi majeruhi .
 
Changamoto nyingine inayowakabili ni chumba cha kuhifadhia maiti kuwa kidogo kwani kina uwezo wa kuhifadhi maiti sita hivyo maiti 26 zipo nje ya uwezo wao.
 
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia machi 25 mwaka huu katika eneo la Kitonga kata ya Mwalusembe wilaya ya humo.
Chanzo cha ajali inadaiwa mwendo kasi wa dereva wa lori katika kilima na kusababisha ajali hiyo mbaya.
 
Simanzi zimetawala katika wilaya hiyo ,ambapo mbunge wa jimbo la Mkuranga, Abdallah Ulega ,aliishukuru serikali ya wilaya chini ya mkuu wa wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga kwa juhudi zake za kusaidia majeruhi na marehemu kupelekwa hospitalini .
 
Ulega alitoa pole kwa wafiwa na majeruhi na kuwaasa madereva waache kuendesha kwa mwendo kasi kwani husababisha ajali zembe.
 
“Naishukuru pia hospitali ya wilaya kwa juhudi zao baada ya kupokea marehemu na majeruhi kuhangaikia kuokoa maisha yao.” alieleza Ulega.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: