Leo tarehe 22 Machi 2018, mimi na viongozi wenzangu waandamizi wa
Chadema tumetakiwa tena kuripoti Polisi.

Tunaokabiliwa na usumbufu huu ni pamoja na: Mhe Vincent Mashinji
(Katibu Mkuu), Mhe. John John Mnyika, Mb na Naibu Katibu Mkuu Bara,
Mhe. Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar; Mhe Halima J.
Mdee, Mb, Mwenyekiti wa Bawacha, Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Mhe.
John W. Heche, Mb, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti (Mara,
Simiyu na Shinyanga) na Mjumbe wa Kamati Kuu; Mhe. Esther N. Matiko,
Mb, Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Mara na Mweka hazina wa Bawacha
Taifa.

Tuna taarifa pia ya kusudio la kumuunganisha Mhe. Peter Msigwa, Mb,
Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa (Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe
na Iringa) na Mjumbe wa Kamati Kuu katika shauri hili.

Historia ya wito: 

Kwa muda wa wiki tano sasa, kufuatia sintofahamu kadhaa zilizojitokeza
katika uchaguzi wa marudio wa Jimbo la Kinondoni, Dar es Salaam na Siha,
Kilimanjaro, tumekuwa tukisumbuliwa kuripoti Polisi kila wiki kwa mashtaka
ambayo hayajawahi kuwekwa bayana.

Katika kampeni na chaguzi hizi, palijitokeza mambo mengi ya ukiukwaji wa
Haki za binadamu, ukiukwaji wa sheria za uchaguzi, matumizi mabaya ya
madaraka ya kiserikali, udhalilishaji na unyanyapaa dhidi ya Vyama vya
Upinzani, mauaji na mateso kwa viongozi wa vyama vya Upinzani na hata
Wananchi wasio na hatia. 

Wakati nenda rudi hii ikiendelea, tuna taarifa (asante teknolojia) kuwa
zinapangwa njama mahususi za kutubambikia viongozi wa Chadema kesi za
Mauaji au Uhaini ili kuhalalisha azma ya Watawala kutuweka mahabusu kwa
muda mrefu, wakidhani kwa kufanya hivyo watakuwa wamefanikisha
kufifisha na hata kuua kabisa uwepo wa Upinzani katika Taifa.

Jitihada hizo ni pamoja na kujaribu kuhusisha viongozi, wanachama na
wapenzi wa chama chetu na tuhuma aidha za Kigaidi, Mauaji na hata
Uhujumu wa Uchumi.

Mkakati huukKitaifa unashinikizwa na Rais John Pombe Magufuli na
kuratibiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa, Dk Modestus
Kipilimba, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, Jeshi la Polisi,
na Ofisi ya DPP.

"Viongozi" hawa, wasaidizi na washirika wao wamejazana matumaini hewa
kuwa vuguvugu la mabadiliko na uhitaji wa demokrasia ya kweli na vita dhidi
ya udikteta katika taifa hili litazimwa kwa "kuwaficha, kuwapoteza na hata
kuwaua" viongozi wa Chadema na wanaharakati wengine wanaoamini katika
uhalisia huu.

Naam, njama hizi zaweza kuua baadhi, kujeruhi baadhi na hata kupoteza
kadhaa! Lakini kamwe, hazitazima njozi za Watanzania wema kupigania haki
na ustawi katika nchi yao.

Naamini kwa kuzima uongozi wa Chadema uliopo leo, siyo tu kutaruhusu
kuchipua kwa kasi kwa uongozi mbadala, bali pia kutaamsha ari ya taifa
kuongeza juhudi katika harakati ili hatimaye kutokomeza udikteta na uongozi
wa kiimla katika nchi yetu.

Taifa lina msiba! Wanasiasa, wanaharakati, wanahabari na hata wasanii
wanateswa, wanafungwa, wanajeruhiwa na wengine kuuwawa!
Wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje wanalia! Viongozi wa dini
wanachanganyikiwa! Wakulima, wafugaji na wavuvi wako hoi! Hata watoto
na wanafunzi nao ni tishio kwa watawala! 
Taifa limejazwa hofu. Wengi hawasemi, lakini wanataabika rohoni.

Wanaisubiri fursa iwavyo vyovyote vile.
Nguvu, majeshi na silaha zao, magereza na mifumo kandamizi haziwezi kuwa
suluhu ya uimla huu. Tuimarishwe badala ya kufifishwa. 

Hatukimbii!! Tuko tayari kwa lolote, popote!
Shime Watanzania! Msitulilie! Lilieni watoto wenu na Taifa la kesho.
Na iwe vyovyote iwavyo! Damu, mateso, dhihaka dhidi ya maisha yetu iwe
chachu ya dhati katika kutafuta Tanzania aliyoikusudia Mwenyezi Mungu
yenye kusimamia haki, demokrasia, usawa, utu na ustawi kwa wote!!
Aluta Continua!!!

Freeman Aikaeli Mbowe
Share To:

msumbanews

Post A Comment: