Gari aina ya Scania  lori lenye namba za usajili T415 DJG  likiwa limechomwa moto na wananchi baada ya kumgonga mwendesha Pikipiki na kusababisha kifo.
Nyuma ya gari ambalo limechomwa Moto likiwa na maandishi ambayo yanayosomeka IMEBAKI STORI.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita,Mponjoli Mwabulambo akizungumza na waandishi wa habari juu ya tukio la wananchi kujichukulia sheria mkononi na kuchoma gari.


NA,JOEL MADUKA,GEITA.


Gari aina ya Scania  lori lenye namba za usajili T415 DJG  limechomwa moto baada ya kumgonga mwendesha pikipiki  na kusababisha  kifo  cha Matha Paulo aliyekuwa ni Muuguzi wa kituo cha afya cha Kaseme Wilayani Geita alikuwa amebebwa kwenye pikipiki hiyo.

Tukio hilo limetokea majira ya saa moja jioni  katika kijiji cha Kasesa kwenye barabara ya katoro-Lunzewe ambapo mwendesha boda boda na abiria wake walikuwa wakitokea mji mdogo wa Katoro,huku watoto wawili akiwemo kichanga cha miezi miwili (2) waliokuwa wamepakatwa na marehemu mama yao wakinusurika kifo.

Akisimulia shuhuda wa tukio hilo Bw,Mayala Bushibe, alisema yeye alikuwa ameongozana na boda boda iliyopata ajali,huku nyuma na mbele yao yalikuwapo magari mawili likiwemo lori yakipishana na mwendesha piki piki alipojaribu kulipita ndipo likawagonga gari hilo.

“Baada ya utelezi wa mvua akayumba  Yule dereva wa boda boda akaanguka na gari la nyuma likampitia ikabidi akimbie Yule boda boda na baada ya kuangalia Yule mtu aliyegongwa tulijua ni nesi wa kaseme”Alisema Mayala.

Josia Thobias ambaye ni mkazi wa Kaseme  alisema tukio la namna hiyo sio la mara ya kwanza kutokea kwani  ajali za hivyo zimeendelea kujitokeza na kwamba ni mara ya pili kutokea.

Kamanda wa polisi mkoa wa Geita Mponjoli mwambulambo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa pikipiki ambaye alikimbia baada ya kutokea kwa ajali,huku akiwataka wananchi kuachana na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: