Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
Mhe.Selemani Jafo (aliyesimama) akitoa hotuba yake kabla ya kuzindua
programu ya wanafunzi walimu kutoka Chuo Kikuu cga Dodoma wanaokwenda
kujitolea kwenye shule za Sekondari na Msingi zilizo karibu na maeneo
wanayoishi.


 Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma Mhe.Davis Mwamfupe
akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kuzindua program ya
wanafunzi walimu wa UDOM wanaokwenda kujitolea kwenye Shule za Msingi
na Sekondari.

Mratibu wa program ya kujitolea kwa Wanafunzi Walimu Dr.Ombeni Msuya
ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma akielelezea namna
walivyojipanga kusimamia program hiyo.

 Mwenyekiti wa Wanafunzi Walimu wanaokwenda kujitolea akizungumza
kwenye uzinduzi wa Programu hiyo iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Shule ya
Sekondari Umonga iliyopo Mjini Dodoma.

 Baadhi ya wanafunzi walimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma wakifuatilia hotuba
ya mgeni rasmi kabla ya uzinduzi wa program maalumu ya kwenda kujitolea
kwenye Shule za msingi na sekondari.

..................................................................................
Nteghenjwa Hosseah, OR-TAMISEMI

Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma wanaosomea Shahada ya Ualimu
wameunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika Utoaji wa
Elimu Msingi bila malipo kwa kujitolea kwenda kufundisha katika shule za
msingi na Sekondari zilizoko katika maeneo yao wakati wa Likizo.

Akizindua mpango huo wa kujitolea kwa wanafunzi walimu zaidi ya 500 Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe.Selemani Jafo
amewataka wanafunzi hao kuwa mfano ya kuigwa kwenye shule
watakazoenda kufundisha ili kuipa heshima zaidi programu hii iweze kuwavutia
walimu wengine zaidi.

Alisema kuwa mnapofika mashuleni mkawe mfano bora kwa wadogo zenu,
mkaonyeshe uwezo wenu katika kufundisha na kuwafikishia yale muhimu
katika masomo yao, mkaonyeshe Umahiri katika Taaluma yenu ndipo kujitoa
kwenu kutaheshimiwa na kuthaminiwa na jamii nzima ya watanzania.

Aliongeza kuwa wanafunzi wa UDOM mnaokwenda kujitolea ndio mtakua
waasisi wa programu hii kitaifa hakuna eneo lolote Nchini ambako wanafunzi
walimu kwa Umoja wao waliamua kwa hiari kwenda kufanya kazi katika jamii
walizotoka tena bila malipo yeyote kwa wengine watakaofanya hivi katika
maeneo yao watakua wameiga kutoka kwenu.

“Huu ni Uzalendo wa hali ya juu na mmejitoa kwa Taifa lenu na kupitia
kujitolea kwenu mnasaidia kutatua changamoto zinazokabili Wizara ya
TAMISEMI hakika mnapaswa kutambuliwa na kuweka kumbukumbu sahihi ya
nani na nani alishiriki katika program hii” Alisema Jafo.

Akizungumza katika Uzinduzi wa kampeni hiyo Meya wa Manispaa ya Dodoma
Mhe.Prof.Davis Mwanfupe amewaasa wanafunzi walimu wanaokwenda
kujitolea na kuwakumbusha kwenda kuitumia vyema Taaluma yao kwa kuwa
Nuru ya kuiangazia jamii katika mambo yale yaliyo mema.

Naye Mratibu wa Programu hii ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Dodoma Dr.Ombeni Msuya amesema huu ni muendelezo wa kampeni ya Nipe
Daftari na Peni, Nami nipate Elimu iliyozinduliwa na Waziri Jafo hivi karibuni.

Amesema sababu ya programu hii inatokana na ukweli kwamba shule nyingi za
Serikali zina Upungufu wa Walimu kutokana na Upatikanaji wa Elimu bure
ambao umeongeza Idadi ya wanafunzi katika shule nyingi kuanzia Msingi hadi
Sekondari hivyo wakaona ni vyema kuratibu wanafunzi walimu waweze
kwenda kuunga Mkono jitihada hizi za Serikali.

Hata hivyo Dr. Abdallah Seni ambaye pia ni miongoni mwa waratibu wa
Programu hii alisema sisi ni sehemu ya wanataaluma na wataalamu, kwa
pamoja tumeazimia kuhamasisha walimu wanafunzi na walimu wengine
wanaofanya kazi nje ya Ualimu, kuitikia wito wa kujitolea kufundisha katika
shule ambazo wapo jirani nazo kama sehemu ya uzalendo na upendo kwa Nchi
yao.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: