Friday, 16 March 2018

Walimu 16 kufukuzwa kazi kwa sababu hii

Picha ya mtandao

JUMLA ya walimu 16 wamefukuzwa kazi wilayani Nkasi mkoani Rukwa kwa kipindi cha miaka mitatu na wengine 11 wamepewa onyo kali baada ya kubainika wametenda makosa mbalimbali.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) wilayani, Richard Katyega, aliyasema hayo jana mbele ya Kamishna wa TSC, Samuel Korosso na kufafanua kuwa katika kipindi hicho walipokea mashauri 23 na kusababisha walimu 16 kufukuzwa kazi, 11 kupewa onyo kali na wengine watano waliondolewa kazini baada ya kubainika kuwa na vyeti bandia.

Alisema katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 na 2018  tume hiyo imeweza kusikiliza mashauri hayo na kuyatolea maamuzi.

Alisema uamuzi ulifanywa baada ya kusikiliza mashauri hayo na bila kumwonea yeyote na kusisitiza kuwa sheria zilizingatiwa.

Katyega alisema tume hiyo pia imekuwa ikiwahamasisha walimu kufuata maadili ya ualimu, ili wasikumbane na adhabu ikiwamo kufukuzwa kazi.

Kwa upande wake, Kamishna Korosso alieleza kusikitishwa na vitendo vya uvunjifu wa maadili kwa baadhi ya walimu, hali iliyosababisha wafukuzwe kazi.

Alisema tume haitasita kuwachukulia hatua walimu watakaobainika kufanya vitendo ambavyo ni kinyume cha maadili ya ualimu.

 Aliwataka walimu kuzingatia misingi ya sheria ya utumishi kwa walimu kama inavyowataka na kuongeza kuwa walimu wilayani humo hawanabudi kuzipitia sheria za utumishi wa walimu zinavyoagiza.

Maofisa kutoka ofisi ya kamishna wa tume hiyo walitoa mada mbalimbali zilizolenga kuwapatia elimu walimu na kuwakumbusha sheria za utumishi wa walimu.

Kwa upande wao walimu walipata fursa ya kueleza changamoto zinazowakabili na walipatiwa majibu.

No comments:

Post a comment