RAIS wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ameridhishwa na dira ya maendeleo ya uongozi wa nchi na anaunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais John Magufuli.

Hayo yalielezwa katika taarifa ya Ofisi ya Makamu wa Rais iliyotolewa jana kwa wanahabari, ikimkariri Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier.

Taarifa hiyo ilisema Balozi Clavier alibainisha hilo baada ya kukutana na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kwa mazungumzo.

Balozi huyo mpya aliongozana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Emmanuel Baudran.

Katika mazungumzo hayo Ikulu jijini Dar es Salaam, imeelezwa Balozi Clavier aliwasilisha salamu za Rais Macron kwa Magufuli na kusema “Rais wa Ufaransa ana uhakika na Tanzania ijayo na anaunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanywa na Rais Magufuli,” taarifa ilisema.

Mbali na kueleza kuwa Balozi Clavier aliipongeza serikali kwa mapambano dhidi ya rushwa na urasimu jambo ambalo litavutia wawekezaji wengi nchini:

Taarifa ilisema balozi huyo, aliipongeza pia Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika masuala mbalimbali ya kimataifa.

“Tanzania ni nchi yenye utulivu na amani kitu ambacho kinaipa taswira nzuri Umoja wa Mataifa.” Balozi huyo alimjulisha makamu wa rais kwamba Ufaransa imekusudia kuimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi na kisiasa na Tanzania, ilisemwa.

Aidha, katika mazungumzo hayo, Ufaransa iliahidi kuanzisha majadiliano mbalimbali katika masuala ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.

FURSA MBALIMBALITaarifa pia ilisema Balozi Clavier alimjulisha Mama Samia kuwa wafanyabiashara kati ya 30 na 40 kutoka Ufaransa watakuja nchini mwezi ujao kujionea fursa za kibiashara na uwekezaji zinazopatikana nchini.

Balozi huyo pia alielezea azma ya Ufaransa katika kushirikiana na vyuo vikuu nchini katika kuanzisha na kuendesha kozi mbalimbali kwa manufaa ya pande zote mbili.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa AFD, Baudran alisema shirika linakusudia kuanzisha kiwanda cha vifaa vya umeme wa jua mkoani Shinyanga baada ya kufanya miradi ya uboreshaji majitaka katika Manispaa ya Temeke.

"Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alimshukuru na kumpongeza Balozi wa Ufaransa kwa kazi nzuri wanazofanya hapa nchini," taarifa ilisema zaidi.

"Alimhakikishia kwamba Serikali ya Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano kwa mambo yote muhimu yenye maslahi kwa wananchi."
Share To:

msumbanews

Post A Comment: