Tuesday, 20 March 2018

Nyavu haramu za milioni 190 zateketezwa

 Picha ya mtandao

NYAVU haramu za uvuvi zenye thamani ya Sh. milioni 187 zimeteketezwa katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.

Zoezi hilo lililofanyika katika mwalo za muyobozi, lilishuhudiwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalla Ulega, ambaye pia alitumia fursa hiyo kusikiliza maoni ya wadau wa sekta ya uvuvi.

Akizungumzia zoezi hilo, Ulega alisema Serikali haina mpango wa kuwaonea wananchi katika utekelezaji wa majukumu yake ukiwamo utoaji wa huduma.

Ulega alisema Serikali inatumia ubunifu wa kisayansi ambao utatatua kero na changamoto zinazowakabili wavuvi kwa kuwajengea uwezo wa elimu sahihi ya zana bora  za uvuvi ili wanapochomewa watambue hasara ya matumizi ya nyavu haramu na faida za matumizi ya nyavu halali zenye macho makubwa.

“Serikali ya Rais Magufuli hainyanyasi wala haina mpango wa kuonea watu, tunatumia taarifa za kisayansi kuondoa kero ya kutotii sheria bila shuruti na msidhani nyavu haramu mnachomewa wavuvi tu,” alisema na kuongeza:

“Tushalipisha faini zaidi ya Sh.milioni 800, kesi za wahujumu uchumi zinaendelea mahakamani, zaidi ya Sh. bilioni moja za wenye viwanda waliokiuka sheria zimeunguzwa moto, hatuonei dagaa tu hata sangara na mapapa wanawajibisha kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ya Idara ya Uvuvi,” alieleza Ulega.

Pia aliwataka maofisa uvuvi watende haki na waepuke urasimu katika kutatua kero zinazoikabili Idara ya Uvuvi na watoe fursa kwa vikundi vya uvuvi vilivyo rasmi kisheria na vikundi vya ulinzi maeneo ya mialo wapewe nyaraka za  kuhitaji zana aina ya mashine za kisasa zenye matumizi kidogo ya mafuta ili wapunguze gharama ya uendeshaji wa mitumbwi ya asili inavyotumia mafuta kidogo.

Aidha, aliwahimiza wadau wa sekta ya uvuvi  Wilaya ya Uvinza watumie mwalo wa kisasa wa Muyobozi unaolinda afya ya mlaji na utaongeza mapato kutoka makusanyo ya fedha kwa mwaka kutoka Sh. milioni 28 hadi Sh. milioni 100 ambazo zitasaidia serikali kutoa huduma bora za kijamii
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: