Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha ameahidi atashughulikia changamoto zinazokikabili Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) ili kukiwezesha Chuo hicho kuanza kudahili wanafunzi.

Naibu waziri Ole Nasha ametoa ahadi hiyo alipofanya ziara ya kukagua shughuli za Maedeleo zinazofanyika katika Chuo hicho kilichopo Wilayani Butiama mkoani Mara.

Ole Nasha amesema Chuo hicho kilianzishwa si tu kwa lengo la kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere lakini pia kuendeleza dhamira yake ya dhati aliyokuwa nayo  kuhusu kilimo.

Akiwa Chuoni hapo Naibu Waziri huyo amebaini kuwepo kwa baadhi ya Watumishi wa Wizara yake wanaosaidia mchakato wa watumishi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere kuhama kwa madai kuwa katika Chuo hicho hakuna kazi za kufanya  jambo ambalo linazidi kurudisha nyuma juhudi za Serikali za kuhakikisha kuwa Chuo hicho kinaanza kazi mapema iwezekanavyo.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Dominick Kambarage amesema Chuo hicho  kimeshindwa kuanza kazi kutokana na kukosa Miundombinu inayokidhi vigezo vya Tume ya Vyuo Vikuu.

Awali kabla ya kutembelea Chuo Kikuu hicho  Naibu Waziri huyo alitembelea  Shule ya Msingi Mwisenge, Shule ambayo amesoma hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere ambapo akiwa shuleni hapo  aliahidi kuwajengea vyumba vitatu vya madarasa.

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

WIZARA YA ELIMU,SAYANSI NA TEKNOLOJIA

3/3/2019

Share To:

msumbanews

Post A Comment: