Wakati idadi ya wagonjwa wa figo ikiendelea kuongezeka nchini, imeelezwa kuwa Tanzania ina madaktari bingwa wa figo 13.

Hayo yameelezwa leo Machi 10, 2018  na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile katika hotuba yake mara baada ya matembezi ya hisani ya umbali wa kilomita 5 kuadhimisha siku ya figo duniani.

"Madaktari bingwa 13 pekee kwa nchi yetu hawatoshelezi, tupo kwenye mikakati ya kuhakikisha tunasomesha wataalamu 100 kila mwaka na tunaanza mwaka huu ambapo wiki ijayo utatoka ufadhili kwa wanafunzi 100," amesema Dk Ndugulile.

Amesema changamoto ni kubwa kwani nchini wanagundulika wagonjwa wengi wapya wa figo, hivyo kuna kila sababu ya Serikali kuandaa wataalamu wengi zaidi ili kutoa matibabu kwa wepesi zaidi.

Rais wa Chama cha Madaktari wa Figo Tanzania, Dk Onesmo Kisanga amesema uchache wa madaktari wa figo nchini upo lakini wanatarajia iwapo Serikali itasomesha wataalamu wengi zaidi wataweza kuwafikia wananchi waliopo pembezoni.

"Tunao madaktari bingwa 13 nchini kwa sasa lakini wawili wengine watamaliza masomo yao mapema mwaka huu na wengine watatu watamaliza mwakani hivyo tunatarajia kuwa na madaktari wapatao 18 ifikapo mwaka 2019," amesema Dk Kisanga.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: