KADA wa Chama cha Wananchi (CUF) ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya chama hicho, Julius Mtatiro, amevuliwa uanachama wa chama hicho na Uongozi wa CUF Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam.

Akitangaza uamuzi huo mapema siku ya Jumapili, Machi 4, 2018, mwenyekiti wa CUF wilaya ya Ubungo, ndugu Bashir Ally Muya, amesema kuwa wamefikia uamuzi huo kutokana na Mtatiro kukaidi agizo la chama hicho lililomtaka kujibu tuhuma mbalimbali zinazomkabili, mbele ya Baraza la Utendaji la Wilaya ya Ubungo.

Muya amedai kuwa, mnamo tarehe 20 Desemba 2017, kamati ya utendaji ya chama hicho iliketi ambapo ilimtaka ndugu Mtatiro, na wenzake sita kuja mbele ya kamati hiyo kujibu tuhuma mbalimbali zinazowakabili, agizo ambalo Mtatiro na wenzake walikaidi.

Ametaja makosa mawili makuu yaliyomfukuzisha uanachama Mtatiro kuwa ni: kutolipia kadi yake ya uanachama kwa muda wa miaka mitatu sasa, kitendo ambacho ni kinyume na katiba ya cha hicho, ambapo inasema endapo mwanachama hatalipia kadi yake ya uanachama kwa muda wa mwaka mmoja pekee, basi mwanachama huyo uanachama wake utasitishwa mara moja.

Ametaja kosa la pili kuwa ni kukihujumu (kukisaliti) chama kwa kushirikiana na Chadema katika chaguzi za marudio zilizofanyika ndani ya wilaya ya Ubungo, ambapo amesema licha ya chama hicho kusimamisha wagombea, Mtatiro na wenzake hawakuwaunga mkono, huku wakitumia muda wao mwingi kuzungumzia masuala ya Chadema.

Aidha, Muya amesema kuwa kwakuwa Mtatiro ni mjumbe wa mkutano mkuu wa taifa,  uongozi wa wilaya utamwandikia barua katibu mkuu wa CUF kumtaarifu juu ya uamuzi huo, ili baadaye aandikiwe barua kutaarifiwa juu ya kufutwa kwake uanachama.

Wengine waliofutwa uanachama ni: Twaha Rashidi, Mwinyi Hamis, Khalid Singano, Jumanne Athuman, Kassim Hamis, na Yusuf Lema.

Miongoni mwa sababu zilizotajwa kuwafuta uanachama ni pamoja na; kuwa na kadi za chama cha Chadema, kumnadi mgombea wa udiwani Kata ya Saranga kwa tiketi ya Chadema kwenye uchaguzi mdogo uliopita ilihali chama hicho kilikuwa na mgombea, pamoja na kumkashifu mwenyekiti wa CUF taifa kwenye mitandao ya kijamii.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: