Mawasiliano yamewaponza RC Mnyeti na Dk Kigwangalla


Machi 8, Mnyeti alitengua agizo la Waziri Kigwangalla aliyewapa miezi tisa wananchi wa Kijiji cha Kimotorok kuondoka katika maeneo wanayoishi wakidaiwa kuvamia eneo la Hifadhi ya Tarangire wilayani Simanjiro.
Wachambuzi wa duru za kisiasa na kijamii nchini wamesema tatizo la mawasiliano ndiyo sababu ya wateule wawili wa Rais John Magufuli; Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla kuonyesha tofauti zao hadharani.
Machi 8, Mnyeti alitengua agizo la Waziri Kigwangalla aliyewapa miezi tisa wananchi wa Kijiji cha Kimotorok kuondoka katika maeneo wanayoishi wakidaiwa kuvamia eneo la Hifadhi ya Tarangire wilayani Simanjiro.
Akizungumza na wanakijiji hao, Mnyeti alisema hakuna atakayekwenda kuwafukuza na kama hilo lipo, yeye ndiye atawaambia wanafukuzwa au la, hivyo wawe na amani.
Mnyeti alitoa kauli hiyo baada ya kusimamishwa na wanakijiji hao alipopita kijijini hapo akielekea katika mkutano wa kuwapokea wanachama zaidi ya 3,000 wa CCM kutoka vyama vingine.
Alisema ofisi ya mkoa inajiandaa kutuma wataalamu kwenda kupima eneo hilo ili kutatua mgogoro.
Februari 25, Waziri Kigwangalla alitoa miezi hiyo kwa wanakijiji na vitongoji vya Massas na Loon’benek wawe wamehama kwa kuwa wamevamia eneo la Hifadhi ya Tarangire.
Katika agizo lake, Dk Kigwangalla alisema kabla ya kuondoka, Serikali itawalipa fidia na watatafutiwa maeneo mengine ikiwa ni pamoja na kujengewa zahanati nje ya hifadhi kutokana na iliyokuwapo kuwa ndani.
Akizungumzia tofauti hizo zilizojitokeza baina ya viongozi hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba alisema tatizo hilo linachangiwa pia na upungufu wa kiuongozi.
Alisema pengine Waziri Kigwangalla alikosea katika mawasiliano lakini RC Mnyeti hakutakiwa kutumia vyombo vya habari katika kutengua kauli yake.
“Busara ya kiongozi inaelekeza kwamba RC alitakiwa awasiliane naye (Dk Kigwangalla) kiofisi, amweleze hatua zinazoendelea na sehemu gani aliyotakiwa kuzingatia kabla ya kutoa tamko lake.
“Halafu waziri pengine angetumia busara kurejea upya kauli yake kwa sababu wote wanatekeleza mipango ya Serikali,” alisema Dk Bisimba.
Profesa wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana alisema tofauti hiyo imechagizwa na ukosefu wa mawasiliano baina ya viongozi hao.
Profesa Bana alisema RC ni ‘rais wa mkoa’ hivyo kwa waziri yeyote anayehitaji kufanya uamuzi ni busara kufanya mazungumzo na RC husika kabla ya kutoa tamko.
“Haiwezekani waziri uingie mkoa fulani na kutoa maamuzi, lazima maelekezo ya waziri yawe yameshapata baraka kutoka kwa mkuu wa mkoa wa eneo husika. Ningeshauri wajenge tabia ya mashauriano ili kuepuka dosari kama hizo. Kwa utaratibu lazima upate ‘briefing’ (maelezo) ya hali halisi na mipango inayoendelea kuhusu jambo husika unalofuatilia,” alisema.
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala bora UDSM, Dk Richard Mbunda alisema pamoja na tatizo la mawasiliano, viongozi hao walihitaji semina elekezi kabla ya kuanza kutumikia nafasi zao.
“Nafasi wanazotumikia kwa sasa ni kubwa, hawakuwahi kuzitumikia tangu waingie kwenye siasa, kwa hiyo inawezekana hawajui athari katika kauli wanazotoa. Semina ingesaidia kujua do’s and dont (mambo ya kufanya na kuacha), kujua direction (mwelekeo) ya rais mwenyewe anataka nini,” alisema.
Alisema kwa madaraka aliyonayo, waziri ana nguvu nchi nzima katika maeneo yanayohusu sekta yake na hufanya uamuzi kupitia vikao vya mawaziri hivyo haikuwa busara kwa mkuu wa mkoa kutengua kauli yake hadharani.
Alisema inatia shaka kwa viongozi kuonyesha wazi tofauti zao na kwamba athari zake itakuwa ni pamoja na kupunguza imani kwa viongozi wa Serikali.
Mkurugenzi wa shirika la Sikika, Irenei Kiria alisema mawasiliano ni tatizo ambalo limewahi kujitokeza si kwa viongozi hao tu, bali hata kwa Rais kutengua uamuzi uliopitishwa na waziri.
Rais Magufuli aliwahi kutengua tamko la Dk Harrison Mwakyembe wakati huo akiwa Waziri wa Katiba na Sheria, baada ya kupiga marufuku wananchi kufunga ndoa bila kuwa na cheti cha kuzaliwa.
“Kwa hiyo tatizo ni mawasiliano, rais ameshafanya hivyo, ni kawaida na inatokea kuwa na mawazo tofauti. Jambo la msingi ni mawasiliano,” alisema Kiria.

Previous Post
Next Post

post written by:

0 komentar: