Mahakama Kuu nchini Kenya imewataka Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Waziri wa Mambo ya Ndani na Kamishna wa Uhamiaji kufika mahakamani leo kujitetea kwanini wasifungwe jela au kulipa faini kwa kuidharau Mahakama.

Jaji wa Mahakama Kuu, George Odunga alisema kuwa maafisa hao wakuu Serikalini walifanya kosa la kuidharau mahakama kwa kukataa wito wa kumfikisha mahakamani hapo mwanasheria Miguna Miguna, Jumatano wiki hii.

Jaji huyo amesema kuwa Mahakama haiwezi kuchezewa na Serikali na haitaruhusu hilo lifanyike kwani ndicho chombo cha haki.

Miguna alishikiliwa na Polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta alipojaribu kurejea nchini humo akitokea nchini Canada alikopelekwa kwa nguvu kwa madai ya kutokuwa raia wa Kenya.

Serikali inadai Miguna aliyekuwa anatuhumiwa kwa uhalifu wa kushiriki zoezi la kumuapisha Raila Odinga kama ‘Rais wa Watu’, alipinga uraia wake mwaka 1988, madai ambayo mwanasheria huyo ameyapinga. Miguna anadai ni raia wa kuzaliwa wa Kenya mwenye uraia pia wa Canada lakini hajawahi kuukana uraia wa nchi hiyo kama inavyodaiwa.

Hata hivyo, mbali na tishio hilo la Mahakama kwa viongozi hao wa vyombo vya usalama, jana usiku Miguna alisafirishwa bila hiari yake hadi Dubai.

Mahakama imewahi kuamuru Muguna aachiwe huru na kama kuna madai yoyote anapaswa kufikishwa mahakamani na sio vinginevyo.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: