LHRC yataja dosari 10 katika uchaguzi mdogo


Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetaja dosari 10 kilichodai zilijitokeza katika uchaguzi mdogo uliofanyika katika majimbo ya Kinondoni na Siha, Februari 17.

Uchaguzi huo ulifanyika kufuatia waliokuwa wabunge wa majimbo hayo, Maulid Mtulia (CUF- Kinondoni) na Dk Godwin Mollel (Chadema- Siha) kujitoa kwenye vyama vyao na kujiunga na CCM.

Wabunge hao waliopitishwa tena kugombea katika majimbo hayo kwa tiketi ya CCM walishinda uchaguzi huo.

Madai ya LHRC yanafanana na yale ambayo yamekuwa yakitolewa na vyama vya upinzani hasa Chadema.

Hata hivyo, juzi mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima aliliambia Mwananchi kwa simu kuwa vyama vya siasa vinapaswa kusoma sheria na kanuni zilizopo ili kuweka mikakati itakayovisaidia kufanikisha malengo yao na kushiriki uchaguzi kwa misingi iliyowekwa. “Hakuna sheria wala kanuni yoyote ya uchaguzi wa rais, wabunge au madiwani inayotaka mawakala wapewe nakala ya kiapo,” alisema Kailima.

Kuhusu malalamiko ya vyama vya upizani ikiwemo Chadema kwa msimamizi wa uchaguzi wa Kinondoni Aaron Kagurumjuli kuwacheleweshea barua za utambulisho na viapo, Kailima alisema; “Msimamizi hakuchelewesha fomu. Alikubaliana na mawakala wote zitolewe Februari 16, saa 12 jioni na ilikuwa hivyo. Wawakilishi wa vyama vyote walikuwepo na walipata nakala hizo.”

Lakini, jana akizungumza na wanahabari, kaimu mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga alitaja suala la mawakala wa vyama vya upinzani kukosa barua na viapo kuwa ni uonevu huku wale wa CCM akidai walipata barua hizo bila usumbufu.

“Kwenye uchaguzi huu waangalizi wa vyama vya upinzani tu ndio waliokosa barua, lakini wa chama tawala walikuwa na barua zao na waliingia mapema kwa ajili ya kufanya uangalizi. Kwa hiyo haikuwa haki na hatuwezi kuogopwa kuitwa Chadema wakati siyo,” alisema Henga.

“Tunasema wazi kabisa wale mawakala walionewa na hawakufanyiwa haki wala halali na ndio maana waliandamana kwenda kudai. Mimi tangu asubuhi niliwaona katika kituo cha Biafra wakihangaika na barua zao hawajaruhusiwa kuingia, lakini wengine wamekaa wako na barua zao.”

Hata hivyo, alisema katika baadhi ya vituo, waangalizi wote waliruhusiwa yaani wa upinzani na CCM.

“Lakini wengi walisumbuliwa, mtu anakuja kuruhusiwa saa nane mchana sasa hapo unaangalia nini na bado saa mbili muda wa kupiga kura uishe?” alihoji.

Kuhusu mawakala wa CCM kupewa hati za viapo mapema, katibu wa Uhusiano wa Kimataifa wa CCM, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga alisema: “Mimi si msemaji wa chama, ila ninachojua wote tulipewa pamoja barua na ilikuwa haki ya kila chama. Kujua nani ambaye hakupewa si rahisi. CCM tulikuwa tunatafuta kura kama wao, kama wanaona haikuwa sawa wanaweza kwenda mahakamani.”

Akifafanua kuhusu alioita unyanyasaji wa mawakala wa vyama vya siasa, Henga alisema kituo chao (LHRC) kilishuhudia siku ya kupiga kura wakizuiwa kuingia kwenye vyumba vya kupigia kura pasipo sababu ya msingi. Alikitaja kituo cha Shule ya Msingi Nasai kwenye Jimbo la Siha akisema mawakala wa chama cha Sauti ya Umma (Sau), Chadema na CUF walizuiwa kuingia kwenye vyumba vya kupigia kura bila sababu ya msingi.

Kuhusu matumizi ya rasilimali za umma kwa masilahi ya vyama, Henga alisema LHRC ilishuhudia baadhi ya mawaziri wakiwa na magari ya Serikali katika kampeni za kumnadi aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk Aloyce Mollel, jambo alilosema ni kinyume cha Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Uchaguzi hasa Sheria ya Gharama za Uchaguzi. Kuhusu matumizi ya watoto katika kampeni, alinukuu kifungu cha 12 cha Sheria ya Mtoto ya 2009 akisema inakatazwa kuwaajiri au kumtumia mtoto katika shughuli yoyote ile ambayo ni hatarishi kwa masilahi mapana ya mtoto, kiafya, elimu, kiakili, kimwili na maendeleo ya maadili.

“Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimeshuhudia video ya mtoto mdogo aliyekuwa jukwaani akitumika kutumbuiza katika mkutano wa kampeni wa CCM uliofanyika Makumbusho Jimbo la Kinondoni Februari 2. Huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu hususani haki za watoto,” alisema.

Akizungumzia matumizi ya nguvu za Jeshi la Polisi wakati wa kampeni na siku ya kupiga kura, aligusia tukio la mauaji ya aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini aliyepigwa risasi wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema walioandamana kudai viapo vya mawakala Jimbo la Kinondoni.

“Sambamba na hilo, Jeshi la Polisi liliendelea kuwashikilia wafuasi 40 wa Chadema wakiwemo wanawake wenye watoto wadogo na majeruhi wawili wa risasi. Kwa upande wa Jimbo la Siha polisi walimpiga mwanamke mmoja na kusababisha kuvunjika mguu,” alisema mkurugenzi huyo.

Katika siku ya kupiga kura, Henga alisema uwepo wa askari wengi wa Jeshi la Polisi wakiwa na silaha za moto uliwatisha wapiga kura.

“Kwa upande wa Jimbo la Siha eneo la Ngarenairobi na Nasai kulishuhudiwa polisi wengi wakiwa vituoni jambo linaloweza kusababisha hofu kwa wapiga kura na kwa kuzingatia tukio la mauaji lililotokea siku moja kabla ya uchaguzi,” alisema.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa alipotafutwa jana kwa njia ya simu kuzungumzia madai ya kuwapo askari wengi wenye silaha za moto, alimtaka mwandishi wa habari hizi kuwatafuta makamanda wa polisi wa mikoa ya Dar es Salaam na Kilimanjaro ambao hata hivyo hawakupokea simu zao kwa muda mrefu.

Hata hivyo, siku moja kabla ya uchaguzi, kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alisema walikuwa wamejiandaa na kuwatoa hofu wananchi watakaoshiriki kwa kuwa polisi pia watakuwa wakizunguka maeneo mbalimbali kuimarisha ulinzi.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa aliwaonya watu kutofanya vurugu akieleza taarifa alizokuwa amezipata za vurugu na kuwataka wananchi kurejea majumbani baada ya kupiga kura.

Kuhusu kupotea kwa sanduku la kura, Henga alisema LHRC ilishuhudia likiondolewa katika kituo cha kupigia kura cha Idrisa Jimbo la Kinondoni na baadaye kurejeshwa na upigaji kura ukaendelea.

Kuhusu hilo, Mkurugenzi wa NEC, Kailima alisema juzi kuwa wakala wa chama chenye malalamiko alitakiwa kujaza fomu namba 14 kuelezea mapungufu hayo.

Henga, alizitaja dosari nyingine zilizotokea siku ya uchaguzi kuwa mwitikio mdogo wa wapiga kura akisema katika majimbo hayo mawili ni asilimia 24 pekee ya waliojiandikisha ndio walipiga kura. Nyingine ni uwezo mdogo wa wasimamizi wa uchaguzi na mazingira yasiyo rafiki kwa wapiga kura wenye ulemavu.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 komentar: