Kocha wa Simba aenda kwao mapumziko


Kocha mkuu wa kikosi cha Simba Mfaransa Pierre Lechantre amekwenda kwao kwaajili ya mapumziko mafupi baada ya timu yake kuondolewa kwenye michuano ya Kombe la shirikisho na Al Masry ya Misri.

Kikosi cha Simba kimerejea nchini jana mchana bila ya kocha Lechantre ambaye ameunganishia Misri kwenda Ufaransa, atakapokuwa kwa muda wa siku kadhaa kabla ya kurejea kibaruani kwaajili ya michuano ya ligi kuu.

Kikosi cha Simba kilirejea na makocha wasaidizi, Mtunisia Mohammed Aymen Hbibi, Mrundi Masoud Juma na mzalendo, Muharami Mohammed ‘Shilton’ na wachezaji wamepewa mapumziko mafupi hadi Jumamosi.

Wachezaji wanne ambao ni kipa Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe na Erasto Nyoni na viungo Said Ndemla na Shiza Kichuya nao walioondokea Cairo kwenda Algeria kuungana na timu ya taifa, Taifa Stars ambayo Alhamisi itacheza mchezo wa kirafiki na wenyeji.

Kwa sasa Ligi Kuu imesimama kwa muda kupisha mechi za kimataifa zilizo katika kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na mechi za Robo Fainali ya kombe la shirikisho nchini (ASFC).
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: