Hatimaye yule mtanzania aliyesaidiwa kupata ufadhili wa matibabu na Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Mhe Paul Makonda amewasili leo hii majira ya saa 9:20 alasiri katika Uwanja wa kimataifa wa Beijing Capital. Mtanzania huyo aitwaye Ahmed Albaity alipokekewa na Maafisa waandamizi wa ubalozi pamoja na watanzania waishio hapa jijini Beijing na kusindikizwa kwenye hospitali ya kimataifa ya Puhua.

Ndugu Ahmed Albaity  ambaye amekuwa akisumbuliwa na tatizo la uti wa mgongo ambalo limedumu kwa takribani miaka kumi na moja akiwa kitandani,tayari ameanza kupatiwa  Matibabu  katika hatua za  awali  mara tu baada ya kuwasili hospitalini hapo.

Mapema akizungumza kwa niaba ya Wanafunzi wakitanzania Wanaosoma na kuishi nchini humo Bw. Remidius Emmanuel ambaye pia ni Katibu Mkuu Shirikisho hilo amesema wao kama watanzania wanaosoma na kuishi katika Taifa la China  wameshiriki kumpokea Mtanzania mwenzao (Ndugu. Ahmed Albaity )  na kwamba  kwa kipindi chote ambacho atakuwepo hapa Beijing China wataendelea kutoa Ushirikiano na kumjulia hali wakati wote.

 "Tunamshukuru Mwenyezi MUNGU amemuongoza Bw.Ahmed kufika salama hapa Beijing, Tumeshuhudia watanzania wakimsindikiza   uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na  kuongozwa na  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe.Paul Makonda, huu ni upendo wa kipekee, na sisi tumeguswa na kuwiwa kumpokea tukiongozwa na Maafisa waandamizi wa Ubalozi wetu hapa China" Alisema Bw. Remidius.

Kwa upande wake ndugu Ahmed Albaity ameushukuru Ubalozi wa Tanzania nchini China pamoja na uwakilishi wa Watanzania wanaosoma na kuishi nchini humo kwa moyo wao wa upendo na namna walivyoweza kumpokea yeye na ujumbe alioambatana nao.

Bw.Michael Semindu moja kati watanzania wanaosoma nchini humo aliyeshiriki mapokezi hayo  alimhakikishia Ndugu Ahmed Ushirikiano kwa kipindi chote atakachokuwa kwenye matibabu jijini Beijing "Nimefurahi kuungana na Maafisa wa Ubalozi pamoja na watanzania wenzangu kumpokea mwenzetu, tunamuahidi ushirikiano kwa kipindi chote atakachoendelea kupata matibabu  nchini China"  Alisema Bw. Michael
Share To:

msumbanews

Post A Comment: