Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi ),Mhandisi Joseph Nyamhanga amewataka wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo na watumishi wote kutimiza wajibu wao kwa kutumia muda wa kazi ipasavyo kwa kufanya kazi kwa bidii.
Ameyasema hayo wakati akizindua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekta ya Uchukuzi leo Mkoani Dodoma.
Aidha Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa Wizara (Sekta ya Uchukuzi) inatambua mchango mkubwa wa wafanyakazi wa ngazi zote katika kufikiwa kwa maamuzi mbalimbali ya kisera na kitaalam na hivyo kufanikisha shughuli za sekta hiyo hali inayochochea Sekta ya Uchukuzi na utabiri wa hali ya hewa kutoa Huduma zenya ubora wa hali ya juu ndani na nje ya nchi.
Akifafanua Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa sekta ya Uchukuzi na Tabiri za Hali ya hewa zinatakiwa kutoa huduma zenye ubora wa kiwango cha juu ndani na nje ya nchi.
“Dhana hii ya ushirikishwaji wa wafanyakazi ni muhimu sana kwa jumuiya yeyote na katika ngazi yeyote,hivyo niwashukuru sana kwa kuzingatia dhana hii muhimu na ninashauri muiendeleze,” Alisisitiza Nyamhanga.
Aidha amewataka wajumbe wa Baraza hilo kuzingatia maelekezo ya kisheria wakati wa kuchangia taarifa muhimu za sekta na kushirikiana katika utekelezaji wake ili kufikia malengo ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi na kusisitiza kuwa Serikali haitosita kumwajibisha mtumishi yeyote ambaye ataonekana kuwa chanzo cha kutotimiza malengo ya bajeti na mpango kazi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi la Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano(Sekta ya Uchukuzi), Dkt.Leonard Chamuriho amesema Wafanyakazi wa Sekta ya Uchukuzi kama walivyo watumishi wengine katika utumishi wa umma wamejipanga kuhakikisha wanafanya zao kwa weledi, uadilifu, juhudi na maarifa katika kutimiza wajibu wao ili kuchangia katika kutekeleza malengo ya Serikali kuwaletea wananchi maendeleo.
“Tunafahamu wazi kwamba kutokusimamiwa na kuendelezwa kwa miundombinu ya uchukuzi na huduma zake hakutowezesha sekta nyingine za kiuchumi na kijamii kukua na kuchangia katika maendeleo ya Taifa,hivyo tutaendelea kuboresha miundombinu ya uchukuzi na huduma zake”,Aliongeza Dkt.Chamuriho.
Uzinduzi wa Baraza hilo ulienda sawia na Uchaguzi wa katibu na Katibu Msaidizi wa Baraza hilo na kinafanyika mjini Dodoma kwa siku mbili kuanzia leo tarehe 21 hadi 22 machi 2018.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: