JESHI la Polisi mkoani Pwani limewaasa madereva hususani wa mabasi yanayofanya safari za mikoani ,kuacha kufanya mbwembwe wakati wakiwa barabarani na kutumia vileo katika kipindi hiki cha sikukuu za Pasaka ili kuepusha ajali zembe.

Aidha jeshi hilo limetoa onyo kali kwa wale wenye nia ya kutenda uhalifu kwenye kipindi hicho .

Akizungumza na waandishi wa habari na baadhi ya maofisa wa jeshi hilo ,kuhusiana na operesheni za kaguzi hizo ambazo ni endelevu ,na kutoa salamu za Pasaka ,kaimu kamanda wa polisi ,mkoani Pwani ,(SSP) Abdi Issango ,alisema madereva wafuate sheria za usalama barabarani bila kushurutishwa .

Amesema wanafanya operesheni ya kukagua madereva wa mabasi hayo na kufanikiwa kuwakamata madereva 29 kwa makosa ya mwendo kasi na kulipita gari la mbele sehemu isiyoruhusiwa (wrong overtaking).

Pamoja na hayo ,Issango alielezea madereva 22 walikamatwa kwa kosa hilo na madereva saba walikamatwa kwa kosa la mwendo kasi .

Alibainisha dereva mmoja alipewa onyo kutokana na kosa lake ,madereva watano waliadhibiwa kwa kulipishwa faini ,na madereva 23 watafikishwa mahakamani kuweza kujibu mashtaka yanayowakabili .

"Katika operesheni hii ,dereva wa kampuni ya basi la Super Feo lenye namba za usajili T.754 DML linalofanya safari zake kati ya Dar es salaam -Songea ,Peter Augustino (38) mkazi wa Makambako "

" Yeye tutamfikisha mahakamani kwa makosa mawili ya kulipita gari la mbele sehemu isiyoruhusiwa  na kuendesha gari akiwa ametumia kileo ambapo baada ya kumpima alikutwa akiwa na kilevi 26.8mg/ml.":;alisema Issango.

Kwa mujibu wa Issango machi 28 mwaka huu jeshi hilo limeendesha msako katika maeneo mbalimbali katika mkoa huo na kufanikiwa kukamamata watuhumiwa 21 wakiwa na bangi kete 155 sawa na gramu 77.5.

Alisema huko Mapinga wilayani Bagamoyo ,walimkamata Wilson Jengua akiwa na mtambo mmoja wa kutengeneza pombe ya moshi(gongo) , "Mbali ya mtambo huo ,tumekamata pombe hiyo lita 62 " alifafanua Issango.

Issango ambae pia ni kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Pwani, alieleza watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka dhidi yao .

Aliwasihi wahalifu wenye mawazo ya kufanya uhalifu kipindi cha Pasaka wabadili mawazo hayo, kabla ya hatari kwani jeshi hilo limejipanga kikamilifu kupambana na uhalifu wa aina yoyote
Share To:

msumbanews

Post A Comment: