Hakimu mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Iringa, John Mpitanjia amesema dhamana ya Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP), Abdul Nondo ipo wazi.

Nondo amefikishwa mahakamani  hapo leo  Jumatatu asubuhi Machi 26, 2018.

Mpitanjia amesema dhamana ipo wazi na Nondo anatakiwa kudhaminiwa na watu wawili ambao ni wakazi wa Iringa, mmoja awe mfanyakazi wa Serikali, na wanatakiwa waweke bondi ya shilingi milioni 5 pamoja na kuwa na mali isiyohamishika.

Kwa sasa wakili wa Nondo, Jebra Kambole anashughulikia dhamana ya mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Nondo anatuhumiwa kwa makosa mawili. Kosa la kwanza ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni Machi 7, 2018 akiwa Ubungo na kusambaza kwa kutumia mtandao wa WhatsApp kuwa yupo hatarini.

Shtaka la pili ni kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa umma mjini Mafinga alipokuwa akitoa taarifa katika kituo cha Polisi Mafinga kuwa alitekwa na watu wasiojulikana jijini Dar es Salaam na kupelekwa Kiwanda cha Pareto cha Mafinga.

Alifikishwa  mahakamani hapo saa tatu asubuhi akiwa kwenye gari la Polisi kisha kupelekwa katika mahabusu ndogo mahakamani hapo na kuingizwa katika chumba cha mahakama saa 3:45 asubuhi. Kesi imeahirishwa hadi Aprili 4, 2018.

Mara ya kwanza Nondo alipofikishwa mahakamani kuliibuka mkanganyiko kwa kisheria kuhusu dhamana baada ya upande wa mashtaka kuomba asipewe kwa maelezo kuwa bado maisha yake yapo hatarini.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: