BAJETI ya harusi ya kifahari ya binti wa bilionea namba moja Afrika kutoka nchini Nigeria, Alhaji Aliko Dangote aitwaye Fatima Dangote, imezua gumzo.

Fatima Dangote alifunga ndoa na rubani Jamili Abubakar, mtoto wa aliyekuwa Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi nchini Nigeria (IGP), Mohammed Dikko Abubakar na kufuatiwa na sherehe ya kihistoria iliyofanyika wikiendi iliyopita jijini Lagos, Nigeria.
Kwa mujibu wa mitandao ya Nigeria, kila chombo cha habari na wamiliki wa mitandao (blogs), wamekuwa wakihaha kupata gharama kamili za shughuli hiyo iliyoweka rekodi ya aina yake.
Wengine wamekuwa wakizungumzia gharama za uwepo wa tajiri namba mbili wa dunia kwa mwaka 2018 kutoka Marekani, Bill Gates kuwa zilifikia hadi zaidi ya shilingi trilioni mbili hivyo kuzidi kuzua gumzo.
“Kama ujio wa Gates tu ni zaidi ya trilioni mbili (jambo ambalo wengi walilipinga), je, gharama za shughuli yote itakuwa kiasi gani?” Alihoji mmoja wa wachambuzi wa tukio hilo kwenye mitandao ya Nigeria.
Mbali na uwepo wa watu wengi wakubwa duniani, pia ishu nyingine iliyosababisha watu kuamini harusi hiyo ilikuwa ni ya bajeti kubwa, ni kitendo cha baba wa bibi harusi, mzee Dangote mwenyewe kumnunulia mwanaye saa aliyovaa iliyokuwa sawa na ya mke wa  
rais iliyogharimu dola za Kimarekani 32,000 (zaidi ya shilingi milioni 70 za Kitanzania).
Wachambuzi hao waliweka wazi kuwa hadi kuhitimishwa kwa zoezi hilo kulikuwa na matukio mengine makubwa yaliyogharimu fedha ndefu kama bridal shower na send-off ya Fatima na shughuli mbili za harusi (receptions) ambazo zilifanywa kwa pamoja na familia zote.
“Ni ngumu kusema bajeti yake ni shilingi ngapi kutokana na ukubwa wa shughuli yenyewe na wapo watu (matajiri) wakubwa waliojitolea kugharamia vitu mbalimbali hivyo kila mmoja anataja kiasi chake kutokana na ukaribu alionao na waandaaji,” alieleza mmoja wa wachambuzi hao.
Mbali na Gates, shughuli hiyo ilihudhuriwa na watu mashuhuri kutoka sehemu mbalimbali duniani akiwemo Rais Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.
Wengine walioudhuria ni pamoja na mke wa rais wa sasa wa Nigeria, Hajiya Aisha Buhari; makamu wa rais wa nchi hiyo, Osinbanjo, spika wa bunge, magavana na watu wengine mashuhuri, wakiwemo wasanii wengi wa muziki na sinema wa Nigeria na wafanyabiashara wenzake wakubwa duniani.
Katika shughuli hiyo, mastaa wa muziki Afrika kutoka Nigeria, Davido na Wizkid waliangusha burudani kali hadi mzee Dangote mwenyewe ikambidi ayarudi.
Ilielezwa kuwa, siri kubwa ya uwepo wa watu hao ni kutokana na ukaribu alionao Dangote na matajiri wenzake, viongozi wakuu wa nchi mbalimbali ambazo amewekeza na upendo wake kwa mastaa kwani naye ni mtu anayependa masuala ya burudani.
Dangote aliyewekeza nchini Tanzania kupitia Kiwanda cha Saruji cha Dangote anashika nafasi ya kwanza kwa utajiri barani Afrika akiwa na utajiri wa Dola za Kimarekani bilioni 12.1 (zaidi ya shilingi trilioni 27 za Kitanzania).
Bilionea huyo ambaye ni mfano wa kuigwa kwa vijana wengi barani Afrika na Tanzania, biashara zake zimesambaa katika nchi nyingi, akisambaza bidhaa nyingi kama sementi na sukari. Dangote alianza biashara yapata miaka 30 iliyopita na bado anaendelea kujitanua kila kukicha.
Wakati anaanza akiwa kijana mdogo, Dangote alikopa fedha kidogo za mtaji kutoka kwa mjomba’ke aliyekuwa amemwajiri ambaye naye alimkopesha kwa makubaliano kuwa azirudishe baada ya miezi mitatu.
Ili kujijengea uaminifu, Dangote alirejesha mkopo huo kabla ya miezi hiyo mitatu kumalizika na tayari alikuwa ameshapata mtaji wa kujitegemea akiwa ameamua kufanya biashara ya bidhaa muhimu kwa maisha ya binadamu ikiwemo sukari na leo ni tajiri namba moja barani Afrika.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: