Wakati afya ya mbunge  wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu inaendelea kuimarika zaidi baada ya kufanyiwa upasuaji wa mfupa kwenye mguu wa kulia jana, familia yake imelalamikia suala upelelezi wa tukio la kujeruhiwa kwake.

Akizungumza mjini hapa juu kuhusu hali ya Lissu, Msemaji wa familia ya Lissu, Wakili Alute Mughwai, amesema hali ya ndugu yao inaendelea na vizuri na wanamshukuru Mungu kwa kila hatua anayopitia katika matibabu lakini hadi sasa hakuna taarifa yoyote waliyopewa kuhusu uchunguzi wa tukio hilo.

“Hakuna taarifa tuliyopewa kama ndugu licha ya kuziomba mamlaka ziombe msaada wa kiupelelezi kutoka nje, lakini tulijibiwa polisi wanaweza kufanya uchunguzi japo hadi sasa hakuna kinachoendelea, wasiwasi wetu ni kwamba polisi hawana utayari wa kuchunguza tukio hili ndiyo sababu wamekuwa kimya,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, Wakili Mughwai amelikumbusha Jeshi la Polisi na mamlaka husika kuhakikisha wanafanya upelelezi wa tukio hilo ikiwamo kuwakamata wahusika.

“Mungu aliye pamoja nasi tunaamini atafunua njia nyingine nasi tuchukue hatua zitakazofuata baada ya kukaa na kushauriana na mgonjwa. Hii tutaifanya pale tutakapoona masuala yamegonga mwamba,” amesema Wakili Mughwai.

Kuhusu mawasiliano na Ofisi ya Bunge kuchangia matibabu ya Lissu ambaye ana haki ya kupatiwa matibabu kutoka kwenye ofisi hiyo, Wakili Mughwai amesema hadi sasa wana zaidi ya mwezi mmoja na siku 15 bila kuwa na mawasiliano na ofisi ya Bunge.

“Familia ilipokea barua ya Bunge Februari Mosi, mwaka huu ikitutaarifu kupokea barua yetu ya Januari kuhusu kuhamishwa kwa Lissu kwenda Ubelgiji kutoka Hospitali ya Nairobi alikolazwa tangu apigwe risasi na kututaarufu kwamba wamewasiliana na Wizara ya Afya iliyotoa madaktari watatu kwenda Nairobi kwa ajili ya kumuona Lissu lakini hawakuweza kumuona kwani tayari alishapelekwa Ubelgiji,” amesema.

Lissu alijeruhiwa kwa risasi Septemba 7, mwaka jana nyumbani kwake mkoani Dodoma kisha kusafirishwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kabla ya kuhamishiwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi
Share To:

msumbanews

Post A Comment: