DC Kinondoni awanyang’anya ofisi wabunge Mdee, Kubenea

Hapi alisema wabunge hao wanapaswa kuwa na ofisi kwenye majimbo yao na si kwenye ofisi yake iliyopo Jimbo la Kinondoni.
Akizungumza mwanzoni mwa wiki, Hapi alisema, “Nimewaondoa ili waende wakakae na wananchi wao huko majimboni. Wanafanya nini kwenye ofisi yangu? Tunataka wabunge wawe karibu na wananchi ili wawatumikie. Isitoshe, hakuna sheria inayotulazimisha kuwapa ofisi.”
Kabla ya Hapi kutafutwa kuzungumzia suala hilo, Mdee kupitia mtandao wa kijamii aliandika waraka akiwataka wananchi wenye shida kumfuata katika ofisi yake binafsi iliyopo jimboni kwake (Kawe) kwa kuwa amefukuzwa kwenye ofisi ya awali.
Alipopigiwa simu kuzungumzia suala hilo, Mdee alisema alipewa barua ya kuondolewa Julai mwaka jana.
Katika barua hiyo ambayo Mwananchi imeiona, ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni inamtaka mbunge huyo kutafuta ofisi yake badala ya kutumia ya Serikali.
Mdee amedai kwamba alifukuzwa baada ya kukosoa hatua ya Serikali kuwakataza wanafunzi wa kike wenye mimba kurudi shuleni baada ya kujifungua.
“Baada ya kupambana na suala la mimba za utotoni nikitaka watoto wa kike warudi shuleni ndipo nikafukuzwa,” alisema.
Alisema baada ya kuandikiwa barua ya kuondoka Kinondoni alipewa ofisi katika Tarafa ya Kawe aliyosema haikumfaa akieleza ilikuwa imejaa masanduku ya kupigia kura na haikuwa na umeme.
“Niliwaandikia barua ya kuikataa ofisi ile na baadaye walinipa nyingine iliyoko Kata ya Mbezi Juu, huko nilikuta ofisi ya container ambayo ilikuwa na watumishi wa kata zaidi ya 10, sikuwa na pa kukaa,” alisema.
Alisema aliiandikia barua ofisi ya Bunge mara tatu akilalamikia kunyang’anywa ofisi lakini hajajibiwa hivyo aliamua kujitafutia ofisi binafsi.
“Hili lilimfika hata mbunge wa Ubungo, Kubenea. Niliwaagiza wasaidizi wangu wahamishie vitu kwenye ofisi yangu binafsi,” alisema.
Kubenea alikiri kuondolewa katika ofisi iliyokuwa jengo la ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na sasa anayo binafsi eneo la Urafiki.
“Ni kweli nimeondolewa lakini nimeshapata ofisi kwenye Jengo la Urafiki karibu na kituo cha Polisi,” alisema Kubenea.
Alisema kwa kuwa yuko Wilaya ya Ubungo, ameshamwandikia barua katibu tawala wilayani humo akitaka apewe ofisi ijapokuwa bado hajajibiwa.
Hata hivyo, mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara alisema wilayani Ilala hakuna usumbufu kwa kuwa wamejengewa ofisi jimboni humo katika Kata ya Pugu.
“Nimejengewa ofisi ipo Kata ya Pugu na wameniwekea samani. Bunge lilishapitisha bajeti ya ujenzi wa ofisi za wabunge mwaka 2016/17,” alisema Waitara.
Mbunge wa Bunda Mjini ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Sera, Uratibu na Bunge, Ester Bulaya alisema alipokea malalamiko ya Mdee na Kubenea kuondolewa kwenye ofisi zao na ameliwasilisha kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama ambaye alimweleza kuwa litashughulikiwa na Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: