DC atoa tamko kwa wamiliki migodi ya Tanzanite


Mirerani. Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Zephania Chaula amesema atawachukulia hatua kali wamiliki wa migodi ya Tanzanite wanaowashawishi wachimbaji wao kutolipwa mishahara na kukubali kupewa asilimia 10 pindi uzalishaji ukipatikana.

Akizungumza leo Machi 5, 2018 katika mji mdogo wa Mirerani, Chaula amesema Serikali haina kauli mbili kwenye jambo moja.

Amesema Serikali ilishatoa agizo la wamiliki wa migodi kuingia mikataba ya kuwalipa mishahara kila mwisho wa mwezi na si kuwapa asilimia 10 baada ya uzalishaji.

Ofisa kazi wa Mkoa wa Manyara, Deodatus Munishi amesema wamiliki wa migodi wanapaswa kuwalipia wachimbaji wao asilimia moja ya mishahara yao ili wanufaike nayo pindi wakipata tatizo.

Ofisa wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Japhet Petro amewataka wamiliki wa migodi kujiunga na mfuko huo na kuwachangia wafanyakazi wao ili pindi wakipata tatizo waweze kunufaika kwa kulipwa fidia.

Mmoja wa wachimbaji wa madini hayo, Charles Mshana amesema Serikali ingepaswa kuwapa muda wamiliki wa migodi ili waweze kufanikisha suala hilo na si kutekeleza kwa ghafla kama ilivyoagiza sasa.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 komentar: