Sunday, 4 March 2018

Dakika 41 za Prison na Mbao kabla ya mechi kuahirishwa


Baada ya jana mchezo wa ligi kuu soka Tanzania Bara kati ya Tanzania Prison dhidi ya Mbao FC kuahirishwa dakika ya 49, kutokana na uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kuzidiwa na mvua, dakika 41 zilizobaki bado ni mtihani.
Dakika hizo 41 zilipangwa zichezwe leo saa 4:00 asubuhi lakini imeshindikana kutokana na Mvua inayoendelea kunyesha jijini Mbeya hivyo kusogezwa mbele tena.
Mchezo huo wa VPL sasa utapigwa saa 10:00 jioni kwa dakika 41 zilizosalia katika dimba hilohilo la Sokoine ambapo pande zote mbili zimekubaliana kufanya hivyo huku pia ikisubiriwa hali ya hewa kama itakuwa rafiki.
Wakati mchezo huo unaahirishwa dakika ya 49 tayari wenyeji Tanzania Prison walikuwa mbele kwa bao 1-0 lilofungwa dakika ya 11 ya mchezo na Mohammed Rashid kupitia mkwaju wa Penalti.
Hadi sasa Prison ipo katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 29 wakati Mbao FC ya jijini Mwanza inashika nafasi ya 12 ikiwa na alama 19.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: