Watu watano wamefariki na wengine kujeruhiwa baada ya basi lililokuwa likisafirisha wakimbizi kutoka Kigoma kuelekea Burundi kupinduka.

Basi hilo lilipata hitilafu katika mfumo wa breki likiwa eneo la K9, Kasharazi-Ngara lenye mteremko na kona kali na kugonga gari lingine lililokuwa pembeni na kisha kupinduka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Agustino Olomi, akizungumzia ajali hiyo amesema miili ya waliofariki dunia bado haijatambuliwa pamoja na idadi ya majeruhi.

Amesema waliofariki dunia ni wanawake watatu na wanaume wawili. Kati yao yupo mkazi wa Kasharazi aliyekuwa akiendesha baiskeli ambaye basi lilimwangukia.

Mmoja wa madereva waliokuwa katika msafara huo, Raymond Revocatus, amesema kila basi lilikuwa na wastani wa abiria 65.

Baadhi ya majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya Murugwanza wilayani Ngara kwa matibabu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: