Wednesday, 21 February 2018

Watu 18 wapoteza Maisha Dodoma


Watu 18 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa wa kipindupindu mkoani Dodoma ndani ya miezi minne huku zaidi ya watu 470 wakiugua ndani ya muda huo.

Hayo yamethibitishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. James Kiologwe na kusema ugonjwa huo tangu uingie Dodoma Oktoba mwaka 2017, hadi sasa umesababisha vifo hivyo na idadi hiyo ya wagonjwa.

"Wagonjwa wengi wanatoka katika wilaya za Mpwapwa na Chamwino na miongoni mwa sababu za kuenea kwa ugonjwa huo ni unywaji wa maji ya kwenye madimbwi ambayo si safi na salama. Ugonjwa huu ulianza Oktoba, mwaka jana, katika wilaya zote za mkoa wa Dodoma lakini zaidi katika wilaya hizo mbili", amesema Dkt Kiologwe.

Pamoja na hayo, Dkt. Kilogwe ameendelea kwa kusema "kuna wakati ulipungua, lakini umerudi tena na umekuja kwa kasi sana mwezi huu wa pili hadi juzi kulikuwa na wagonjwa wapya 26 na 22 kati yao waliruhusiwa kurudi nyumbani na wanatoka Mpwapwa na Chamwino".

Kwa upande mwingine, Dkt. Kiologwe amesema wanaendelea na jitihada za kukabiliana na ugonjwa huo kwa kugawa ‘Water Guard’ vidogo 250,000 kwa ajili ya kusafisha maji na kuweka katika vyanzo vya maji huku akiwata wakazi wa mkoa huo kuhakikisha wanachemsha maji ya kunywa na kuzingatia kanuni zote za usafi, ili kuepukana na ugonjwa huo.
Previous Post
Next Post

post written by:

0 comments: