Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limewakamata vijana watatu maeneo ya Mwanjelwa, Kata ya Ruanda Tarafa ya Iyunga Jijini Mbeya wakiwa na nyara za serikali ambazo ni vipande vinne vya meno ya Tembo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoani humo DCP Mohammed Mpinga amesema mnamo Februari 05, 2018 majira ya 1:45 usiku walifanikiwa kuwakamata vijana hao waliotambulika kwa majina ya Kenedy Lupembe Simsokwe (43) ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha SAUT tawi la Mbeya na mkazi wa Iyela, Mathew Elikana Mwanjala (42) mpiga picha pamoja na Shaban Mkwiche (24) mkazi wa Iyunga.

Aidha, Kamanda Mpinga amesema baada ya kukamatwa na kupekuliwa watuhumiwa hao walikutwa na nyara hizo ambavyo vina uzito wa kilogram 5 vyenye thamani ya Tshs Milioni 33.

Kwa upande mwingine, DCP Mpinga amesema taratibu za kisheria zinafanyika ili watuhumiwa wafikishwe mahakamani kwa hatua zaidi, huku akiwataka wananchi kuacha tabia ya kuwa na tamaa ya kujipatia utajiri wa haraka kwa kutumia njia za mkato zisizo halali, badala yake wafanye kazi halali ili kupata kipato halali.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: