Wananchi wakazi wa halmashauri ya Arusha wametakiwa kutambua umuhimu wa kulipa ushuru na kodi  elekezi na kufahamu kuwa mapato hayo hutumika kwenye shughuli za maendeleo katika maeneo yao na taifa kwa ujumla.
Rai hiyo imetolewa na wajumbe wa baraza la madiwani wakati wa mkutano wa baraza hilo wa kujadili taarifa za maendeleo kwa kipindi cha robo ya pili uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa halmashauri hiyo.
Madiwani hao wametoa rai hiyo wakati wa kujadili agenda ya kupitisha mapendekezo ya sheria ndogo za ushuru wa halmashauri hiyo kwa lengo la kukusanya mapato ya ndani agenda iliyokuwa na mijadala yenye mivutano mingi.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha Mheshimiwa Noah Lembris amesema kuwa ifike wakati kila mwananchi  kutambua umuhimu wa kulipa kadi na ushuru na kutambua kodi hizo hukusanywa kwa ajili ya maendeleo ndani  ya halmashauri yao.
Ameongeza kuwa halmashauri inaendeshwa kwa mapato ya ndani yanayotokana na kodi na ushuru unaotozwa kwa wananchi na kuongeza kuwa asilimia sitini ya mapato hayo yanarudi kwenye kata na vijiji kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
" Kodi na ushuru unaokusanywa kwenye maduka, masoko na maeneo mbalimbali zinatumika kuendesha halmashauri na asilimia sitini inarudi vijijini kutekeleza shughuli na miradi ya maendeleo kwa faida ya wananchi wenyewe hivyo ni vema wananchi kulipa bila kukwepa" amesema Mwenyekiti Lembris
  Naye Diwani wa kata ya Musa Mheshimiwa Florah Zelothe amesema kuwa hakuna namna halmashauri inaweza kuendeshwa bila kuwa na mapato hivyo ni vema waheshimiwa madiwani kuwaelimisha wananchi kuwa na tabia ya kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo katika maeneo yao.
Awali Madiwani hao katika mkutano huo licha ya kupitia mapendekezo ya Sheria hizo za Ushuru wamejadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo kwa kipindi cha miezi mitatu na kuweka mipango mikakati ya utekelezaji wa shughuli hizo kwa robo ijayo ya tatu.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: