Thursday, 15 February 2018

Wafanyabiashara wa Nyama Arusha wailalamikia TRA


CHAMA cha wauzaji wa nyama jiji la Arusha,(Wanjamuco)kimelalamikia Mamlaka ya Mapato TRA mkoani hapa kwa kuwapandishiwa  kodi ya mapato Mara dufu kutoka kiasi cha shilingi 318,000 hadi kufikia  shilingi milioni 1 kwa mwaka .

Wakiongea jana kwenye kikao cha pamoja kilichoketi katika machinjio ya jiji la Arusha(Arusha meet) wakati wakipatiwa elimu ya matumizi sahihi ya mashine za kielektroniki(EFDs) na umuhimu wa kulipa kodi na maofisa wa kodi wa TRA.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao,Alex Lasiki alisema kimsingi kiwango hicho ni kikubwa na kinawaumiza sana wao kama wafanyabiashara ukizingatia kwamba wametakiwa kuanza kutumia mashine za EFDs wakati wa mauzo ya nyama kwa kila bucha na kwamba jana februali 14 ,mwaka huu ilikuwa ni siku ya mwisho kufanya biashara hiyo bila kuwa na mashine ya EFDs.

 Wameiomba TRA kuangalia uwezekano wa kuwapunguzia kiwango hicho cha kodi na kufikia walau sh,600,000 kutokana na kwamba biashara  ya nyama niyakubahatisha na nyama huwa inapungua uzito kila wakati.

‘’Unajua kiwango tuliochoapewa kulipa cha shilingi milioni moja ni kikubwa sana hii biashara yetu ya nyama tunanunua ng’ombe kwa kumkadilia uzito na mara nyingi unapoenda kupima kwenye mizani baada ya kumchinja unakuta kilo sio zenyewe na hivyo unapata hasara’’alisema 

Wakizungumza kwa niaba ya wenzao mfanyabiashara Richard Mboya ,Medeus Masawe ,Humfrey Minja wamesema kuwa biashara ya nyama wanaifanya kwa makadirio na wanapokuja kumchinja ng’ombe unakuta amekata kilo jambo ambalo linapelekea  baadhi yao kupata hasara.

Wameishauri serikali kuangalia upya utaratibu wa kuuza ng’ombe kwa kutumia mizani ili kuondoa ukadiriaji ambao baadae umekuwa ukiwapatia hasara pindi wanapoenda kuchinja ng’ombe.

Akijibu kauli za wafanyabiashara hao,Afisa Kodi wa TRA mkoa wa Arusha,Marliseri aliwaeleza wafanyabiashara hao taratibu za mabadiliko ya kodi kwamba mfanyabiashra mwenye mtaji wa kuanzia sh,milioni 7.5 hadi milioni 11.5 atapashwa kulipa kodi ya sh,318,000 kwa mwaka.

Aidha mfanyabiashara mwenye mtaji wa sh,milioni 11.5 hadi milioni 16 atapaswa kulipa sh, milioni 546,000 kwa mwaka na mwenye mtaji wa sh,milioni 16 hadi 20 atapaswa kulipa sh,milioni 862,000 kwa mwaka.

Aliwataka wafanyabishara hao kuanza kutumia mashine za EFDs kwenye mabucha yao  kama njia pekee itakayowaondolea utata baina yao na mamlaka ya TRA na kwamba baadhi ya malalamiko yao likiwemo suala la kodi yatafanyiwa kazi.

No comments:

Post a comment