Kampuni inayotoa huduma katika mradi wa mabasi yaendayo haraka (Udart) imepokea mabasi 70 kutoka China ambayo yataongeza nguvu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 16, 2018 wakati wa kupokea mabasi hayo yaliyokuja na meli ya MV Treasure katika Bandari ya Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Udart, Charles Newe amesema ujio wa mabasi hayo utaifanya kampuni hiyo kuwa na mabasi 210.

Newe amesema mabasi hayo ambayo kila moja gharama yake ni dola 260, yatakuwa na uwezo wa kubeba abiria 150 hadi 160 yatasaidia pia katika kuongeza ajira, kuimarisha uchumi wa Tanzania na kurahisisha hali ya usafiri katika Jiji hilo.

“Bado kuna watu walikuwa wanatumia magari binafsi kutokana na magari yetu kujaa, lakini ujio wa mabasi haya naamini utawafanya wayaache nyumbani magari yao na kupunguza gharama kutoka Sh8,000 hadi Sh2,000 kwa siku kwa ajili ya usafiri binafsi,” amesema.

“Pia itasaidia kupunguza gharama za uendeshaji , kwani kutokana na kubeba abiria wengi kupita kiasi yamejikuta yakiaharibika mara kwa mara na badala ya basi kukaa miaka nane, linakaa miaka minne.”

Amesema pamoja na kuongezeka kwa mabasi hayo, utaratibu wa abiria kusimama utaendelea kwa kuwa ndio usafiri wa majiji katika miji yote duniani.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: