Na: Veronica Kazimoto,Arusha


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata na kutaifisha bidhaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na tani moja ya sukari na chumvi, majani ya chai mifuko 18, mirungi kilogramu 16, vifaranga vya kuku 5000 na mayai kasha 416 katika mpaka wa Namanga mkoani Arusha zikitokea nchini Kenya kupitia njia zisizo rasmi.

Akizungumza mara baada ya kukamata bidhaa hizo, Meneja Msaidizi wa Forodha mkoani hapo Edwin Iwato alisema bidhaa hizo ni mali ya Joseph Sekino, Innocent Minja na Andrew Lyimo wote wakiwa ni wafanyabiashara kutokea Tanzania na watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.

“Tumewakamata wafanyabiashara watatu ambao ni Joseph Sekino akiwa amepakia tani moja ya sukari na chumvi na majani ya chai mifuko 18 kwenye gari Na. T 785 AWV, Innocent  Minja akiwa na mayai kasha 416 na mirungi kilo 16 kwenye gari Na. T 443 CQU na Andrew Lymo akiwa na vifaranga vya kuku 5000 kwenye gari Na. T 441 DHW wote wakitokea nchini Kenya kuja mkoani Arusha,” alisema Iwato.

Iwato alieleza  kwamba, wafanyabiashara hao waliingiza baadhi ya bidhaa hizo kwa kutumia vifungashio vya bidhaa nyingine za nchini Tanzania ili kuficha uhalisia wake huku wakiwa hawana vibali wala kulipa ushuru wa Serikali kama inavyotakiwa.

Alifafanua kuwa, mirungi ilikamatwa ndani ya mifuko ya plastiki maarufu kama Rambo ikiwa imefichwa kwenye boneti ya mbele ya gari aina Noah Na. T 443 CQU sehemu ya injini.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Richard Kayombo alisema, tabia ya wafanyabiashara hao siyo tu inawahujumu wafanyabiashara wenzao bali inakwamisha azma ya Serikali ya kukusanya mapato kwa ajili ya maendeleo ya kila mwananchi.

“Tabia ya wafanyabiashara hawa siyo nzuri kwa kuwa inakwamisha ukusanyaji mapato ya Serikali na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ili iwe fundisho kwa wengine wanaofikiria kufanya biashara pasipo kutumia njia rasmi na kulipa ushuru ipasavyo”, alisema Kayombo.

Aidha, Kayombo aliongeza kuwa, bidhaa zote haramu zilizokamatwa zitateketezwa kwa mujibu wa Sheria, zile zinazofaa kwa matumizi ya binadamu zitagawiwa kwa taasisi mbalimbali za Serikali zenye uhitaji kwa mujibu na taratibu zilizowekwa na TRA na magari yote yaliyotumika kusafirisha bidhaa hizo yametaifishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Utaifishaji wa magari na bidhaa ambao usafirishaji wake haufuati sheria na taratibu, unalenga kukomesha shughuli za magendo nchini ambazo kwa kiasi kikubwa zinakwamisha juhudi za Serikali katika ukusanyaji wa mapato.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: