Changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Jiji la Mwanza kuwa historia baada ya Serikali kuanza utekelezaji wa ujenzi wa miradi mikubwa miwili ya maji yenye thamani ya sh. bilioni 112.

Hayo yamesemwa leo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akizungumza na viongozi na watendaji wa Halmashauri za Jiji la Mwanza, Ilemela na Nyamagana akiwa katika siku ya sita  ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.

Waziri Mkuu amesema miradi hiyo inahusisha kuboresha upatikanaji wa maji katika maeneo ya pembezoni wenye thamani ya sh. bilioni 75 ambao utahusisha ujenzi wa chanzo kipya cha maji kwenye eneo la Butimba chenye uwezo wa kutoa lita milioni 40 kwa siku.

Ametaja maeneo yatakayonufaika na mradi huo kuwa ni Butimba, Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Sawa, Lwanhima, Kishiri, Nyahingi, Luchelele, Malimbe, Bulale, Fumagila, Usagara, Kisesa, Buswelu, Nyamwilolelwa, Kahama, Nyamadoke, Nyamhongolo, Mondo, Kiseke, Kangae, Meko, Nsumba na Bulola.

Waziri Mkuu amesema mradi mwingine ni wa kuboresha upatikanaji wa maji katika maeneo ya milimani wenye thamani ya sh. bilioni 37 ambao ulianza kutekelezwa Februari, 2017 na unatarajiwa kukamilika Agosti 2018.

Amesema wakazi 105,649 wanaoishi katika maeneo ya milimani hususan yaliyo juu ya matenki ya maji ambayo hayapati huduma kwa sasa watanufaika. Maeneo hayo ni Nyasaka, Bugarika, Nyegezi, Capripoint, Mjimwema, Nyakabungo na Kitangiri.

Ameongeza kwamba Serikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini watapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: