Umoja wa Ulaya (EU) umetoa tamko kuhusu matukio ya utekaji na mauaji yanayotokea nchini, ukiitaka Serikali kufanya uchunguzi wa kina.

Taarifa ya umoja huo uliyotolewa leo Februari 23, 2018 inaeleza kuwa imetolewa na ushirikiano wa mabalozi wa nchi wanachama wa umoja huo wenye uwakilishi Tanzania na kuungwa mkono na mwakilishi na mabalozi wa Norway, Canada na Uswisi.

“Tunashuhudia kwa wasiwasi mwendelezo wa matukio ya hivi karibuni yanayotishia nidhamu ya kidemokrasia na haki za Watanzania, katika nchi iliyojizolea umaarufu mkubwa duniani kwa utulivu, amani na uhuru.”

“Tumesikitishwa na kifo cha mwanafunzi aliyepigwa risasi mwisho wa juma lililopita Akwilina Akwilini, anayeombolezwa nchi nzima. Tunakaribisha wito wa Rais John Magufuli wa uchunguzi wa haraka,” inaeleza taarifa hiyo.

Katika taarifa hiyo EU imetoa wito wa uchunguzi wa kina kwa vifo vyote vya wanaharakati wa kisiasa na haki za binadamu.

“Tunatoa pole za dhati kwa familia zao zote. Tuna wasiwasi na ongezeko la ripoti za ukatili katika miezi ya hivi karibuni, kama vile, jaribio lililohatarisha maisha ya mbunge Tundu Lissu; kupotea kwa watu kama mwandishi wa habari Azory Gwanda na mashambulio yaliyopoteza uhai wa viongozi wa Serikali,” inaeleza EU.

Umoja huo umesema pia yametokea matukio yaliyowahusisha wawakilishi wa vyombo vya usalama na wananchi Mkoa wa Pwani ndani ya miaka miwili iliyopita.

“Tunaungana na Watanzania katika kuwaomba wahusika wote, kutunza amani na usalama wa michakato ya kidemokrasia, watu wake na kuheshimu utawala wa sheria bila udhalimu.”

Akwilina alipigwa risasi Februari 16,2018 eneo la Kinondoni Mkwajuni, wakati Polisi wakiwatawanya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakielekea ofisi za msimamizi wa uchaguzi wa ubunge Jimbo la Kinondoni kudai viapo vya mawakala wao.

Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), alipigwa risasi Septemba 7,2017 nje ya makazi yake mjini Dodoma. Kwa sasa yupo nchini Ubelgiji akiendelea na matibabu.

Azory ni mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), aliyetoweka tangu Novemba 21, 2017 Leo ametimiza siku 95 tangu alipopotea.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: