Ikiwa kwenye msimu wake wa kwanza tangu irejee ligi kuu klabu ya Singida United, imezidi kuonesha njaa ya vikombe kwenye msimu wake wa kwanza, baada ya leo kufanikiwa kushinda mchezo wake wa FA dhidi ya Polisi Tanzania.

Mchezo huo uliopigwa kwenye uwanja wa Namfua mjini Singida jioni ya leo, Singida United imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 hivyo kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo, ambayo bingwa wake anapata nafasi ya kuwakilisha nchi.

Mabao ya Singida United jioni ya leo yamefungwa na Juma Kennedy dakika ya 70 pamoja na Tafadzwa Kutinyu dakika ya 77 na kuimaliza Polisi Tanzania ambayo imesafiri kutoka jijini Dar es salaam.

Singida United sasa imekuwa timu ya pili kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ya shirikisho, ikitanguliwa na Njombe Mji ambayo ilifuzu kwa kuiondoa timu ya Mbao FC ambayo ilicheza fainali msimu uliopita na kupoteza mbele ya Simba.

Baadae kuna mchezo mwingine wa 16 bora, Azam FC watakuwa nyumbani kwao Azam Complex kucheza na KMC ya Kinondoni. Yanga wenyewe watashuka dimbani kesho dhidi ya Majimaji ya Songea.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: