siku 3 za kufa na kupona za kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Kinondoni na Siha zinazotarajiwa kumalizika Jumamosi ya Februari 17 mwaka huu ambapo vyama vitatu vikubwa vya siasa; CCM, Chadema na CUF vinapambana.
Wakati CCM ikitamba kuibuka na ushindi katika majimbo hayo kwa madai kuwa serikali yake imetekeleza yale iliyoahidi, Chadema imesema haitakubali kuchezewa kama ilivyokuwa katika uchaguzi wa kata 43 wa Novemba 26 mwaka jana.

Changamoto zilizoibuka katika uchaguzi huo wa madiwani zilisababisha vyama vinavyounda Ukawa ambavyo ni Chadema, NLD, CUF na NCCR-Mageuzi kususia uchaguzi mdogo wa ubunge wa Longido, Songea Mjini na Singida Kaskazini uliofanyika Januari 13, uamuzi ambao uliungwa mkono na vyama vingine vya Chaumma kinachoongozwa na Hashim Rungwe na ACT- Wazalendo kinachoongozwa na Zitto Kabwe.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema juzi katika mahojiano na gazeti hili kwamba chama hicho tawala kitashinda katika chaguzi hizo huku akitaja sababu mbili; “Tunashughulikia shida za wananchi na tunafanya siasa za maendeleo.”
Alisema CCM imejipanga kushinda na itafanya hivyo kwa sababu ni chama kinachoeleweka zaidi kwa wananchi.
Chadema nao wamesema watashinda na hawatakubali kuhujumiwa kama ilivyokuwa kwenye kata 43.
Akizungumzia uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema: “Kitawaka, hatutakubali kuchezewa kama ule uchaguzi wa kata 43, tunataka haki itendeke la sivyo hakitaeleweka.”

Alipoulizwa watatumia njia gani kushinda, Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alisema: “Hatuwezi kuweka silaha zote hadharani, lakini niseme tu kwamba hatutakubali kuchezewa.”

Salum Mwalimu akifanya kampeni.

Vita ya kuwania Jimbo la Kinondoni tumeshuhudia Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu akipambana na mgombea wa CCM, Maulid Mtulia (pichani) ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CUF kabla ya kuhamia chama hicho Desemba 2, mwaka jana hivyo kupoteza sifa ya kuwa mbunge.

Lakini pia wananchi wameshuhudia mapambano makali kati ya Chadema na mgombea wa CUF, Rajabu Salim Juma anayeungwa mkono na chama hicho kinachoongozwa na Profesa Ibrahim Lipumba.
Tayari Jumaa ameilalamikia Chadema kwa uamuzi wake wa kumsimamisha Mwalimu kwa madai kuwa unavunja nguvu ya upinzani kuibuka na ushindi.

Patashika ngingine mwingine katika siku hizi tatu zilizobaki ni baina ya CUF upande wa Lipumba ambaye anatambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kama mwenyekiti halali wa chama hicho, dhidi ya CUF upande unaomuunga mkono katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ambao wamemuunga mkono mgombea wa Chadema kwa mwavuli wa Ukawa.
Katika Jimbo la Siha nako vita itakuwa kali siku tatu zilizobaki kati ya mgombea wa Chadema, Elvis Mosi na wa CCM, Dk. Godwin Mollel ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema tangu 2015 mpaka Desemba 14 mwaka jana alipojivua uanachama na kuhamia CCM.

Pamoja na uchaguzi huo kuwa katika majimbo mawili, Kinondoni ndiko kunakotarajiwa kuwa moto na Mtulia anaonekana kuwa na kibarua kigumu zaidi kwani anaingia katika uchaguzi huo akikabiliwa na upinzani kutoka makundi mawili ambayo yote yalimuunga mkono na kushirikiana mpaka alipotangazwa mshindi kwa kumbwaga aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan.
Kibarua cha kwanza ni CUF upande wa Maalim Seif ambao kwa kiasi kikubwa walipigania ushindi wake sambamba na kumpitisha kwa mwamvuli wa Ukawa.

Mvutano ulioibuka katika chama hicho baada ya Profesa Lipumba kurejea kwenye uongozi mwaka 2016, ikiwa ni mwaka mmoja tangu alipoutangazia umma kwamba amejiuzulu uliibua makundi mawili ndani ya chama hicho, ambayo yamechuana vikali katika uchaguzi huo moja likiwa upande wa Chadema.
Pia, uwepo wa Juma, mgombea huyo wa CUF ambaye mwaka 2015 alikuwa meneja wa kampeni wa Mtulia, kunaweza kumpa wakati mgumu mgombea huyo wa CCM.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: