Kaimu Mkurugenzi wa TFDA, Agnes Kijo
Serikali kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini Tanzania (TFDA) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini, imepiga marufuku matangazo ya biashara za vipodozi na dawa za kuongeza maumbile kwenye mitandao ya kijamii kama vile Instagram, Facebook, Twitter na kwenye blogs.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Februari 18, 2018 jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa TFDA, Agnes Kijo amesema matangazo hayo yanatakiwa kukoma mara moja na wahusika wanastahili kufika katika mamlaka hizo kuomba kibali.
Bi Kijo amesema kumekuwepo na wimbi la watu mbalimbali wanaotangaza vipodozi kwa lengo la kujichubua na dawa za kuongeza maumbile kwenye mitandao hiyo ya kijamii wakifanya kinyume na Sheria ya Mamlaka ya Chakula, Dawa na Vipodozi sura ya 219.
Amesisitiza kuwa matangazo ya vipodozi na dawa hizo yamekuwa na madai mbalimbali kama vile kuongeza makalio, kuongeza nyonga, sehemu za siri za mwanaume, kurudisha bikira kwa wanawake na kuondoa mabaka sugu na tiba hizo kwenye mfumo wa vidonge, jeli, losheni, mafuta, krimu na dawa za kunywa. Kijo alisema baadhi ya watu wamekuwa wakipotosha umma kuwa bidhaa zao zimethibitishwa na TFDA kitu ambacho si kweli.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: