Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amemtaka kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Arnord Msuya kumsimamisha kazi Ofisa Tarafa ya Dongobesh, Bayo Banka kwa madai ya kushindwa kutekeleza wajibu wake kutokana na kuchanganya siasa na kazi.
Pia, amewataka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ambao hawaungi mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kuacha kazi vinginevyo atawachukulia hatua kwa kutotimiza wajibu wao ipasavyo na kuingiza siasa kazini.
Mnyeti ametoa agizo hilo jana Februari 5,2018 wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo katika ziara yake ya siku saba. 
Amesema Banka anapaswa kusimamishwa kazi hadi hapo atakapotoa maelezo ya kushindwa kutimiza wajibu wake kwa kuchanganya siasa na kazi. 
Amebainisha kuwa CCM ilifanyika kampeni na kuinadi Ilani yake ya uchaguzi kwa wananchi, kwamba kinachofanyika sasa ni utekelezaji wa Ilani hiyo kwa watumishi kuwatumikia wananchi.
"Mnakaa ofisini na kulipwa mishahara na posho nyingi lakini mnashindwa kuwatumikia wananchi badala yake mnaingiza siasa chafu. Natoa onyo kwa wote msirudie jambo hilo hata mara moja nitawachukulia hatua kali,"amesema Mnyeti. 
Mnyeti amesema anayo majina na taarifa za baadhi ya watumishi wanaofanya kazi kizembe na kuzorotesha  shughuli za Serikali.
"Pamoja na ofisa tarafa huyo,  pia nakukabidhi majina mengine ya watumishi ambao wanatekeleza maagizo ya viongozi wa vyama vingine vya kisasa badala ya kutekeleza maagizo ya viongozi wa Serikali inayoongozwa na CCM," amesema Mnyeti. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga amesema watumishi wa halmashauri hiyo wamejipanga kuhakikisha wanawatumikia wananchi ipasavyo. 
USISAHAU KU LIKE PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI
Share To:

msumbanews

Post A Comment: